TANZANIA

Askari aliyemuua mwanahabari nchini Tanzania mwaka 2012 afungwa jela miaka 15

Mahakama Kuu mjini Iringa nchini Tanzania imemhukumu jela miaka 15 askari wa kikosi cha kuzuia ghasia Picifius Simon, kwa kosa la kumuua bila kukusudia mwanahabari  Daudi Mwangosi mwaka 2012.

Polisi wakimpiga mwahabari Daudi Mwangosi
Polisi wakimpiga mwahabari Daudi Mwangosi
Matangazo ya kibiashara

Mwanahabari huyo alipoteza maisha wakati polisi walitumia nguvu kuwasambaratisha wafuasi wa chama cha upinzani CHADEMA Wilayani Mufindi, wakati alipojikuta katika ghasia hiyo wakati akifanya kazi yake.

Mauaji hayo yalizua maandamano makubwa ya wanahabari jijini Dar es salaam, kutaka polisi waliohusika kuchukuliwa hatua na kulinda uhuru wa wanahabari nchini humo.

Jaji wa Mahakama hiyo Paul Kihwelo amesema ushahidi uliowasilishwa Mahakamani umebaini kuwa polisi huyo alitenda kosa hilo.

Aidha, Jaji huyo amesema askari huyo alikiri kuwa alitekeleza mauaji hayo bila kudhamiria.

Hukumu hii inamaliza miaka minne ya kusubiri haki kwa familia ya Mwangosi na wanahabari nchini Tanzania.