SUDAN KUSINI

Ban Ki Moon amwonya rais Kiir kuhusu uteuzi wa Jenerali Gai

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon RIJASOLO / AFP

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amemwonya rais wa Sudan Kusini Salva Kiir kutokana na hatua yake ya kumteaua Jenerali Taban Deng Gai kuchukua nafasi ya Riek Machar kama Makamu wa kwanza wa rais wa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Moon amesema, hatua hiyo inaweza kusababisha mgogoro mkubwa wa kisiasa na kiusalama nchini humo na hivyo kwenda kinyume na mkataba wa amani uliotiwa saini kati ya rais Kiir na Machar kuunda serikali ya mpito mwaka uliopita.

Msemaji wa Moon, Farhan Haq amesema uteuzi wowote wa kisiasa nchini humo ni lazima uendane na mkataba huo wa amani.

Machar aliondoka jijini Juba mapema mwezi huu baada ya kuzuka kwa mapigano mapya kati ya vikosi vyake na vile vya Kiir jijini Juba na haijulikani yuko wapi.

Uteuzi wa Gai unakuja wiki moja tu baada ya Machar kumfuta kazi kama Waziri wa madini baada ya kuonekana kushirikiana kwa karibu na upande wa Kiir.