BURUNDI-USALAMA

Baraza la Usalama laidhinisha kupelekwa kwa polisi 228 nchini Burundi

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana limekubaliana kupeleka kikosi cha polisi wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi, hiyo ikiwa ni hatua yake imara hadi sasa kujaribu kumaliza vurugu za zaidi ya mwaka mmoja sasa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa
Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa UN Photo/Loey Felipe
Matangazo ya kibiashara

Baraza hilo limepitisha azimio lililoandaliwa na Ufaransa kuhusu kupeleka hadi polisi 228 wa Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa Bujumbura na maeneo mengine ya nchi kwa kipindi cha awali cha mwaka mmoja.

Burundi imesema haitakubali zaidi ya polisi 50 wa Umoja wa Mataifa, jambo linalo ibua swali kuhusu ikiwa kikosi hicho kilichopendekezwa kitakuwa na nguvu katika idadi ya kuleta mabadiliko nchin humo.

Hata hivyo nchi nne wanachama wa Baraza hilo la Umoja wa Mataifa hazikupiga kura kuidhinisha pendekezo hilo ambalo lilipitishwa na wajumbe 11 pekee.

Nchi ambazo hazikupiga kura ni pamoja na China, Misri, Angola na Venezuela, ambazo zimeeleza kuwa ipo haja ya kupata ridhaa ya Bujumbura kwa ajili ya kikosi hicho cha polisi kupelekwa nchini Burundi.