SUDANI KUSINI

Umoja wa Mataifa waombwa kuunga mkono kikosi cha Ukanda Sudan Kusini

Mamia ya watu wa Sudan Kusini wamekimbilia katika kituo cha Umoja wa Mataifa mjini Juba
Mamia ya watu wa Sudan Kusini wamekimbilia katika kituo cha Umoja wa Mataifa mjini Juba REUTERS/UNMISS/Handout via Reuters

Marekani imetoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana Ijumaa kuunga mkono kikosi cha kikanda kitakacho pelekwa nchini Sudan Kusini kwa ajili ya kusaidia kuongeza nguvu kwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa UNMISS ambao wameshindwa kukabiliana na vurugu nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Baraza la Usalama lilipitisha azimio la kuongeza muda wa kuhudumu kwa kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, hadi Agosti 12 ili kuruhusu muda wa kujadili hatua zingine za kuidhinisha kikosi kipya.

Azimio hilo pia linatarajia kuweka vikwazo vya silaha nchini Sudan Kusini na vikwazo dhidi ya wale wanaoonekana kuhusika na vurugu.

Balozi wa marekani kwenye Umoja wa Mataifa Samantha Power amesema pendekezo la ukanda wa IGAD linastahili kuungwa mkono na baraza la usalama.

Mji wa Juba ulikumbwa na mapigano makali kwa siku kadhaa mapema mwezi Julai baina ya vikosi tiifu kwa serikali na vile vinavyomtii aliyekuwa kiongozi wa waasi wa zamani Riek Machar.

Karibu watu 300 wamepoteza maisha katika vurugu hizo na walinda amani wawili raia wa China waliokuwa wakilinda amanai chini ya UNMISS waliuawa katika shambulizi kwenye kambi ya Umoja wa Mataifa UN ambako maelfu ya raia hukumbilia kwa ajili ya usalama.