Maafisa wa IEBC wasema watajibu baadhi ya madai yanayowakabili
Imechapishwa:
Kamati maalum inayochunguza utendakazi wa Makamishena wa Tume ya Uchaguzi nchini Kenya, imetupilia mbali madai ya Tume hiyo kuwa haina mamlaka ya kuwaondoa Ofisini.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo James Orengo amesema, Kamati hiyo ina haki ya kusikiliza mamalamishi yote kuhusu Makamishena hao na kutoa uamuzi utakaolenga kuboresha utendakazi wa Tume hiyo.
Aidha, Kamati hiyo imewaambia Makamishena hao kuwa wana uhuru wa kujibu au kutojibu shutuma zilizowasilishwa dhidi yao kuhusu uhuru wao wa kufanya kazi.
Hata hivyo, Makamishena hao wamesema watawasilisha nyaraka za kujitetea mbele ya Kamati hiyo.
Mapema hivi leo, Makamishena wa IEBC, waliiambia Kamati hiyo kuwa haikuwa na mamlaka yoyote ya kuwaondoa Ofisini.
Mwenyekiti wa Tume hiyo Issak Hassan alihoji uhalali wa kamati hiyo kisheria na kusisitiza kuwa Katiba, inaeleza kuwa tume hiyo unaweza kuondolewa tu Ofisini ikiwa hoja maalum utawasilishwa bungeni kujadiliwa na kupigiwa kura.
Mazungumzo haya ya siku 30 yalikuja baada ya maandamano ya wiki kadhaa ya muungano wa upinzani CORD kutaka mazungumzo ya kuwaondoa Ofisini Makamishena hao kwa madai kuwa walikuwa wanaipendelea serikali na baadhi yao ni mafisadi.
Kamati hiyo imekuwa ikipokea maoni kutoka kwa mashirika ya kiraia, viongozi wa dini, wanasiasa, watalaam wa sheria na wananchi wa kawaida, na inavyoonekana imeafikiwa kuwa ni lazima Makamishena hao waondoke Ofisini.