SUDAN KUSINI

Wanajeshi wa Machar watishia kuushambulia mji wa Juba, hofu yatanda

Ndege ya kivita ya jeshi la Sudan Kusini ikifanya doria kwenye jiji la Juba hivi karibuni baada ya kuzuka kwa mapigano mapya
Ndege ya kivita ya jeshi la Sudan Kusini ikifanya doria kwenye jiji la Juba hivi karibuni baada ya kuzuka kwa mapigano mapya REUTERS/Stringer

Wanajeshi watiifu kwa makamu wa kwanza wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar, wametishia kuushambulia mji wa Juba, ikiwa kikosi maalumu cha tatu hakitatumwa nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Machar, James Gadet amesema kuwa, kwa sasa wanasubiri amri kutoka kwa amiri jeshi mkuu wao ili waingia Juba.

Gadet ameongeza kuwa mapigano yanaendelea kaskazini magharibi mwa mji wa Juba, na kwamba vikosi vyake vimefanikiwa kuchukua kambi ya jeshi ya Katigir.

Msemaji huyo amesema kuwa, jeshi la Serikali ya Rais Salva Kiir, limetekeleza mashambulizi ya anga kwenye kambi yao iliyoko kaunti ya Lanya, na kwamba makabiliano ya ardhini waliyadhibiti.

Vikosi vya Machar pia vimeripoti mpaka sasa, kufanikiwa kupora magari na vifaru zaidi ya 21 kutoka kwa wanajeshi wa Serikali.

Kwenye taarifa yake, Gadet amekanusha madai ya hivi karibuni ya vyombo vya habari, kuwa kiongozi wao amekimbia nchi ya Sudan Kusini, badala yake amesisitiza kuwa Machar na wakuu wengine wako kwenye maeneo ya Juba.

Hata hivyo msemaji wa Serikali, Ateny wek Ateny, ametupilia mbaliu madai ya vikosi vya upinzani kuwa watashambulia mji wa Juba, akidai kuwa vikosi vya Machar havina huo uwezo.

"Kama ingekuwa rahisi kwao kushambulia mji wa Juba, wangekuwa wamekwishafanya hivyo kitambo sana." Alisema Ateny.

Ateny ameongeza kuwa lengo la Riek Machar ni kuchukua madaraka kwa nguvu, lakini hataweza kufanya hivyo na hana uwezo, huku akidai kuwa Machar anajificha kwenye misitu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Afrika ya kati.

Licha ya kuripotiwa kwa mapigano kwenye maeneo mbalimbali ya nchi ya Sudan Kusini, Serikali inasisitiza kuwa bado iko tayari kutekeleza mkataba wa amani uliotiwa saini na viongozi wao.

Haya yanajiri wakati huu baraza la usalama la umoja wa Mataifa likijadili uwezekano wa kutuma wanajeshi zaidi nchini Sudan Kusini kulinda usalama wa wananchi na wafanyakazi wake.