SUDAN KUSINI

Rais Kiir awafuta kazi Mawaziri wanaomtii Machar

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir REUTERS/Stringer

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir, amewafuta kazi Mawaziri wanne waliokuwa wanaendelea kumtii aliyekuwa Makamu wa kwanza wa rais Riek Machar.

Matangazo ya kibiashara

Kiir ametangaza kuwa nafasi ya Mawaziri hao itachukuliwa na wale wanaomtii Makamu mpya wa rais Taban Deng Gai.

Televisheni ya taifa nchini humo SSBC imetangaza kuwa rais Kiir amewafuta kazi Mawaziri hao Mary Alfonse Nadio Lodira, Mabior Garang, Dak Duop Bishok na Peter Adwok Nyaba.

Mmoja wa Mawaziri aliyeteuliwa na Kiir ni pamoja na Ezekiel Lol ambaye aliwahi kuwa Balozi wa Sudan Kusini nchini Marekani lakini pia mfungwa wa kisiasa mwaka 2013.

Lol sasa ndio Waziri mpya wa Petroli.

Mawaziri wengine wapya ni pamoja na:- Gabriel Duop Lam (Waziri wa Kazi), Gabriel Thok Deng (Waziri wa Madini), Yien Tut (Waziri wa Elimu ya Juu ) na Sofia Gai (Waziri wa Maji na Maliasili).

Wabunge 50 waliokuwa wameteuliwa na Machar wamefutwa kazi na wengine wapya wanaomtii Gai wameteuliwa.

Bunge linatarajiwa kukutana kwa mara ya kwanza siku ya Alhamisi katika kikao muhimu cha kumteua Spika.