SUDAN KUSINI

UN yasema wanajeshi wa rais Kiir waliwabaka wanawake wa kabila la Nuer

Wanajeshi wa SPLA wa Sudan Kusini
Wanajeshi wa SPLA wa Sudan Kusini theinsider

Tume ya Umoja wa Mataifa ya kutetea haki za Binadamu, inashtumu wanajeshi wa serikali ya Sudan Kusini kwa kuwauwa watu wa kabila la Nuer.

Matangazo ya kibiashara

Aidha, Umoja huo unasema jeshi la rais Salva Kiir liliwabaka wanawake na wasichana katika jiji kuu Juba, baada ya  kuzuka kwa vita vipya mapema mwezi uliopita.

Ripoti zinasema kuwa, wanajeshi hao walikuwa ni kutoka kwa kabila la rais Kiir la Dinka.

Watu zaidi 300 walipoteza maisha katika mapigano hayo mapya na kusababisha zaidi ya wengine 60,000 kukimbilia nchi jirani ya Uganda.

Mkuu wa Tume hiyo Zeid Ra'ad Al Hussein amesema wasichana na wanawake 217 kutoka kabila la Nuer la mpinzani wa rais Kiir, Riek Machar walibakwa kati ya Julai tarehe 8 na 25 mwezi uliopita.

Hali ya wasiwasi imeendelea kushuhudiwa jijini Juba, baada ya kuzuka kwa mapigano hayo mapya na hatua ya rais Kiir kuwafuta kazi Mawaziri wa Machar ambaye aliondoka Juba na nafasi yake kuchukuliwa na Taban Deng Gai.