KENYA

Rais Kenyatta asisitiza umuhimu wa reli ya kisasa licha ya kukosolewa

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akizungumza wakati wa mkutano na wadau wa miundombinu, jijini Nairobi, Agosti 8, 2016
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akizungumza wakati wa mkutano na wadau wa miundombinu, jijini Nairobi, Agosti 8, 2016 Kenya Govt

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Jumatatu ya wiki hii amewashukia wakosoaji wake wanao hoji uwiano wa ujenzi wa reli ya kisasa pamoja na miundo mbinu mingine, huku akiwaambia kuwa, ujenzi wa reli hiyo utaendelea licha ya kile kinachosemwa.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza jijini Nairobi, kwenye mkutano wake na wadau wa miundombinu, Rais Kenyatta ametetea uwekezaji mkubwa alioufanya kwenye mradi huo ambao umesababisha nchi yake kuingia madeni, akisema ni muhimu kwa kuimarisha uchumi wa nchi.

“Miundombinu ni muhimu ikiwa nchi yetu inataka kukua na kama tunataka kufikia malengo na matarajio yetu kama watu na kama taifa. Hatuwezi kukimbia ukweli huu,” Rais Kenyatta aliwaambia wajumbe waliohudhuria mkutano huo.

Uwekezaji uliofanywa na Serikali umeendelea kuhojiwa sio tu na wanasiasa wa upinzani lakini hata wananchi wa kawaida, ambao walimuuliza waziri wa Usafiri na uchukuzi James Macharia, kama ilikuwa sahihi kiuchumi kukopa shilingi bilioni 327 za Kenya kujenga reli ya kisasa wakati ingekuwa rahisi kufanya ukarabati wa reli iliyopo?

Maswali haya yameibuka siku chache tu baada ya kuchapishwa kwa jarida la kiuchumi, lililohoji faida na mrejesho wa miradi kama hiyo.

Wadau wa miundombinu waliokutana na Rais Uhuru Kenyatta, ikulu ya Nairobi, Agosti 8, 2016
Wadau wa miundombinu waliokutana na Rais Uhuru Kenyatta, ikulu ya Nairobi, Agosti 8, 2016 Kenya Govt

Katika majibu yake, waziri Machari, amesema ujenzi wa reli hii utaounguza uzito wa mizigo inayosafirishwa kwa njia ya barabara na kunusuru barabara za nchi hiyo, kupunguza foleni na kurahisisha usafiri wa bidhaa.

Rais Kenyatta ametolea mfano mafanikio yaliyopatikana kwenye za Asia kama vile Korea Kusini na Singapore na mashariki ya mbali ambazo zilitoka kuwa masikini na kuwa mataifa yenye nguvu kutokana na ujenzi wa reli za kisasa.

“Nataka niwaulize swali dogo tu wale ambao wanatukosoa kama nchi na kama bara kuhusu uwekezaji wa aina hii. Wako wapi leo hii? Yako wapi hayo mataifa? Bila shaka ni miongoni mwa mataifa yanayokua kwa kasi duniani.

“Walidharau benki ya dunia, waliidharau IMF. Leo hii wanazo benki zao wenyewe, benki za maendeleo zinazokuza uchumi wao,” alisema Rais Kenyatta.

Mkutano huu ulikuwa ni wazo la Rais Uhuru Kenyatta kukutana na wadau kupata mtazamo wao kuhusu barabara, bandari, reli, viwanja vya ndege pamoja na mambo mengine yanayohusiana na tenda, bajeti na namna ya kuwekeza fedha.

Nchi ya Kenya ililazimika kukopa kiasi cha shilingi za Kenya bilioni 327 kutoka Serikali ya China kwaajili ya kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Nairobi na kuongezwa hadi Naivasha.