KENYA-SIASA

Wanasiasa nchini Kenya bado hawajakubaliana kuhusu Makamishna wapya wa IEBC

Nembo ya IEBC
Nembo ya IEBC

Ni mwaka mmoja kuelekea uchaguzi Mkuu mwaka ujao nchini Kenya lakini Kamati maalum ya Bunge ambayo imekuwa ikisikiliza utendakazi wa Tume ya Uchaguzi IEBC, bado haijakubaliana kuhusu njia ya kuwateua Makamishena wapya.

Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo, kamati hiyo ya wanasiasa wa upinzani na serikali imekubaliana kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Uchaguzi Ezra Chiloba, ataendelea kuhudumu katika Tume hiyo.

Imekubaliwa pia kuwa uchaguzi ujao utafanyika tarehe 8 mwezi Agosti mwaka 2017 na matokeo ya urais, yatangazwa katika vituo vya kupigia kura.

Wiki iliyopita, Makamishena wa IEBC walikubali kuachia nyadhifa zao baada ya tuhma mbalimbali ikiwemo ufisadi na madai ya kuipendelea serikali.

Wabunge wa serikali wanataka Tume hiyo kuongozwa na kiongozi wa dini na kuteuliwa na Tume maalum, lakini upinzani CORD unataka Mwenyekiti wa Tume hiyo kuteuliwa na mashirika ya kiraia.

Kamati hiyo inatarajiwa kufikia mwafaka kufikia mwisho wa wiki hii na kuwasilishwa bungeni kujadiliwa na kupitishwa na wabunge.