SUDAN KUSINI

Sudan Kusini yakataa pendekezo la kupelekwa kwa wanajeshi elfu 4, Juba.

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, ambaye Serikali yake imekataa kupelekwa kwa wanajeshi wa ziada zaidi ya elfu 4.
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, ambaye Serikali yake imekataa kupelekwa kwa wanajeshi wa ziada zaidi ya elfu 4. Charles Atiki Lomodong / AFP

Serikali ya Sudan Kusini imelikataa pendekezo la umoja wa Mataifa la kutumwa kwa wanajeshi wa ziada zaidi ya elfu 4 kwenda mjini Juba kuwalinda raia, kwa kile Serikali inasema kupelekwa kwa wanajeshi hao, kunaingilia uhuru wa kujitawala.

Matangazo ya kibiashara

Pendekezo hilo lililowasilishwa na Marekani kwenye baraza la usalama la umoja wa Mataifa, linaomba kupelekwa kwa kikosi maalumu cha wanajeshi watakaokuwa chini ya umoja wa Afrika, kitakachoruhusiwa kutumia nguvu itakapohitajika ili kuhakikisha usalama na kuzuia mashambulizi dhidi ya kambi na ofisi za umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini.

Lakini Serikali ya Juba imelikataa pendekezo hili, ambapo kupitia msemaji wa Serikali, Michael Makuei, amesema wanalikataa pendekezo hilo kwa sababu moja kubwa, kwamba ikiwa wanajeshi hao watapelekwa taifa lao halitakuwa huru kwakuwa litakuwa chini ya uangalizi wa watu wengine na hawakubali hilo.

Makuei amesema kuwa, pendekezo hili ambalo litaongeza pia muda wa tume ya umoja wa mataifa nchini humo hadi mwezi December, litashusha hadhi ya taifa hilo.

Riek Machar akiwa na mpinzani wake Rais Salva Kiir, baada ya kutia saini mkataba wa amani, Mei 9, 2014
Riek Machar akiwa na mpinzani wake Rais Salva Kiir, baada ya kutia saini mkataba wa amani, Mei 9, 2014 REUTERS/Goran Tomasevic

Bodi ya jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki, IGAD, ambayo awali ndiyo ilipendekeza kikosi hicho, ilitangaza kupokea ruhusa ya kupeleka wanajeshi maalumu mjini Juba.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kukataliwa kwa pendekezo hili na Serikali ya Juba, pamoja na kukubali kuhudhuria mkutano wa wakuu wa IGAD, ilikuwa njama ya Sudan Kusini kupoteza muda.

"Kikosi cha ulinzi kilipaswa kuwa huru na sio chini ya tume ya umoja wa Mataifa UNMISS, ili kukiwezesha kufanya kazi zake kikamilifu kama ilivyokubaliwa awali." alisema Makuei.

IGAD ilipendekeza kupelekwa kwa wanajeshi wake mjini Juba ambao watakuwa chini ya tume ya umoja wa Mataifa iliyoko kwa sasa, kikiwa na mamlaka kama yale yaliyotolewa kwa kikosi kilichopelekwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC.

Mji wa Juba ulikumbwa na mapigano makali kwa siku kadhaa kuanzia mwanzoni mwa mwezi Julai mwaka huu kati ya vikosi vya rais Salva Kiir na vile vya aliyekuwa makamu wa kwanza wa Rais Riek Machar.

Watu zaidi ya 300 wameuawa toka kuzuka kwa mapigano mwezi Julai, huku watu zaidi ya elfu sabini wakiripotiwa kukimbia nchi yao.