TANZANIA-SIASA

Chama tawala nchini Tanzania, chasema hakiungi mkono maandamano

Msemaji wa chama tawala nchini Tanzania, Christopher Ole Sendeka
Msemaji wa chama tawala nchini Tanzania, Christopher Ole Sendeka RFI

Chama tawala nchini Tanzania, CCM, kimesema haikuingi mkono maandamano yaliyopangwa kufanywa na upinzani tarehe Mosi ya mwezi ujao, na kwamba wao pia walitamani kufanya mikutano ya kisiasa lakini wanatii agizo la jeshi la Polisi.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa chama tawala, Christopher Ole Sendeka, amewaambia wanahabari jijini Dar es Salaam, kuwa chama chao hakiungi mkono maandamano yaliyopangwa kufanywa na upinzani, na kuongeza kuwa wanaungana na Polisi kupiga marufuku maandamano hayo.

Ole Sendeka amekosoa mkakati wa upinzani aliowatuhumu kuwa hauungi mkono vita ya Rais John Pombe Magufuli ya kupambana na ufisadi uliokuwa umekita mizizi kwenye taifa hilo kwa kutafuta ajenda nyingine, inayojaribu kupoteza uelekeo mzuri wa nchi chini ya utawala wa Magufuli.

CCM inasema kuwa haki ya kuandamana ina uwajibikaji na kwamba wao pia walitamani sana kufanya mikutano ya kisiasa na maandamano kumpongeza Rais kutokana na kasi aliyoanza nayo, lakini hawawezi kufanya hivyo kwa kuwa wanaheshimu amri halali iliyotolewa na jeshi la Polisi nchini humo.

Wananchi wakiwa katika moja ya mikutano ya kampeni nchini Tanzania, 2015
Wananchi wakiwa katika moja ya mikutano ya kampeni nchini Tanzania, 2015 RFI/blog

Ole Sendeka ameeleza chama chake kusikitishwa na ukaidi wa upinzani licha ya kuelekezwa na vyombo vya usalama kuwa zuio la maandamano hayo limetokana na sababu za kiusalama na pia maelekezo ya Rais.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa maandamano ya umoja wa Vijana yaliyokuwa yamepangwa kufanyika mwishoni mwa juma, hayatafanyika tena na badala yake, chama chao kimeamua kutekeleza wito uliotolewa na jeshi la Polisi.

Kuhusu mazungumzo yaliyoitishwa na msajili wa vyama vya siasa kati ya tarehe 29 na 30 ya mwezi huu, msemaji huyo amesema wao kama vyama vingine vya siasa wameupokea wito huo na kwamba ikiwa wataalikwa watashiriki mazungumzo hayo kwa lengo la kupata suluhu na kutanguliza maslahi ya nchi mbele.

Rais wa Tanzania, John Magufuli
Rais wa Tanzania, John Magufuli REUTERS/Sadi Said

Kauli ya CCM inatolewa wakati huu ambapo Alhamisi ya wiki hii, viongozi wa juu wa chama cha upinzani cha CHADEMA, waliitisha mkutano na wanahabari na kueleza msimamo wao, kuwa mikutanok ya kisiasa waliyopanga kuifanya tarehe Mosi ya mwezi ujao iko palepale.

Upinzani umeita kampeni yao kama “UKUTA” wakisema inalenga kuwahamisha wananchi kutambua haki zao za kidemokrasia pamoja na kupinga kile inachokiita ni utawala wa kiimla ulioko madarakani.

Upinzani wenyewe unahoji uhalali wa kisheria ulio nao jeshi la Polisi nchini Tanzania, kuamua kupiga marufuku mikutano ya kisiasa pamoja na ile ya ndani ambayo ilikuwa ikifanywa na baadhi ya vyama baada ya ile ya hadhara kupigwa marufuku.

Kumekuwa na hali ya sintofahamu kuelekea maandamano hayo ya upinzani, ambapo juma hili, jeshi la Polisik limekuwa likifanya , mazoezi ambayo yametafsiriwa na walio wengi kuwa ni vitisho kwa wananchi ambao watashiriki kwenye maandamano hayo ya upinzani, mtazamo ambao jeshi la Polisi inasema ni mazoezi ya kawaida na hayana uhusiano wowote wa kuelekea kwenye maandamano hayo.