TANZANIA

Chama Kikuu cha upinzani nchini Tanzania chaahirisha maandamano ya Septemba Mosi

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA Freeman Mbowe
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA Freeman Mbowe tabelltz.com

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA, kimeahirisha maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika nchini humo tarehe 1 mwezi Septemba kulalamikia kile kinachosema ni uongozi wa  “kidikteta” kutoka kwa rais wa nchi hiyo John Magufuli.

Matangazo ya kibiashara

Mwenyekiti wa Chama hicho Freeman Mbowe amesema kuwa baada ya viongozi wa chama hicho kufanya mazungumzo na viongozi wa dini, wamefikia uamuzi huo ili kutoa nafasi kwa viongozi hao kuzungumza na rais Magufuli kuhusu madai yao na kuonya kuwa ikiwa mwafaka hautafikiwa, wataandamana tarehe 1 mwezi Oktoba.

Mwishoni mwa juma lililopita na mwanzoni mwa juma hili, viongozi wa juu wa chama hicho cha upinzani walikamatwa na Polisi wakati wakiwa wanafanya vikao vyao vya ndani, ambapo walihojiwa kwa saa kadhaa kabla ya kuachiwa kwa masharti.

Jeshi la Polisi nchini Tanzania linasema limejipanga kuhakikisha nchi inakuwa salama, na kuwatoa hofu wananchi kuhusu uwezekano wa kufanyika kwa maandamano hayo, likisema halitakubali watu wachache wavunje amani ya nchi kwa kufanya maandamano yaliyokatazwa.

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, Dar Es Salaam, 5 November 2015
Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, Dar Es Salaam, 5 November 2015 AFP Photo/Daniel Hayduk

Juma moja lililopita, jeshi la Polisi lilifanya mazoezi iliyosema yalikuwa ni mazoezi ya kawaida ya jeshi hilo katika kupima weledi wa vijana wao kukabiliana na maandamano, mazoezi ambayo upinzani uliyatafsiri kama kitisho kwa wananchi.

Viongozi wa dini pamoja na msajili wa vyama vya siasa waliingilia kati mvutano huu, ambapo walikubaliana kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kujaribu kuzungumzia sintofahamu iliyojitokeza.