UFARANSA-UGANDA

Ufaransa na Uganda zatia saini mkataba wa kushirikiana kijeshi

Rais wa Uganda Yoweri Museveni akikaribishwa na wanajeshi katika Ikulu ya rais jijini Paris
Rais wa Uganda Yoweri Museveni akikaribishwa na wanajeshi katika Ikulu ya rais jijini Paris Daily Moniter

Ufaransa na Uganda zimesaini mkataba wa ushirikiano wa kijeshi baada ya rais Yoweri Museveni kuzuru jijini Paris siku ya Jumatatu  na kukutana na rais Francois Hollande.

Matangazo ya kibiashara

Ufaransa sasa itasaidia Uganda katika mafunzo mbalimbali ya kijeshi lakini pia kuwauzia silaha, kutoa mafunzo ya kiiteljensia miongoni mwa maswala mengine ya kiusalama.

Mbali na utiaji saini wa mkataba huo, rais Hollande ameipongeza Uganda kwa kuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha kuwa kuna amani, utulivu na usalama katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Aidha, amesema anatambua kazi kubwa ambayo Uganda inaendelea kuifanya hasa kwa kutuma vikosi vyake vya kijeshi nchini Somali, kwenda kupambana na kundi la kigaidi la Al Shabab, kupitia jeshi la Umoja wa Afrika AMISOM.

Uganda ndio nchi yenye wanajeshi wengi nchini Somalia, ikiwa na wanajeshi zaidi ya 6,000 katika kikosi hicho cha wanajeshi cha zaidi ya elfu 21.

Mbali na suala la Somalia, viongozi hao wawili wamezungumzia mzozo wa kisiasa nchini Burundi, ambao rais Museveni ndio msuluhishi mkuu.

Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yamekuwa yakihusika na mzozo huu, lakini kwa mujibu wa ripoti iliyowasilishwa kwa viongozi wa mataifa hayo hivi karibuni jijini Dar es salaam nchini Tanzania, upande wa serikali na upinzani nchini Burundi hawatoi ushirikiano unaohitajika.

Rais Hollande amekubali kuzuru Uganda pindi tu akapoalikwa na rais Museveni.