SOMALIA-KENYA

Al-Shabab washambulia kituo cha polisi kaskazini mashariki mwa Kenya

Kundi la wapiganaji wa kiislamu wenye silaha, usiku wa kuamkia Alhamisi ya September 22, wameshambulia kituo kimoja cha Polisi Kaskazini mashariki mwa nchi ya Kenya, jirani kabisa na mpaka wa nchi ya Somalia, polisi wamethibitisha.

Mwanajeshi wa Kenya katika Chuo Kikuu cha Garissa, ambapo shambulizi la kundi la Al Shebab kuotoka liliwaua watu 148, Aprili 2 mwaka 2015.
Mwanajeshi wa Kenya katika Chuo Kikuu cha Garissa, ambapo shambulizi la kundi la Al Shebab kuotoka liliwaua watu 148, Aprili 2 mwaka 2015. © AFP PHOTO / CARL DE SOUZA
Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa jeshi la polisi nchini Kenya, George Kinoti amethibitisha kutokea kwa tukio hili na kuongeza kuwa, wapiganaji zaidi ya 50 waliojihami kwa silaha walivamia kituo cha polisi na polisi waliokuwa doria, ambapo baadae polisi hao walifanikiwa kukabiliana nao.

Polisi inasema kuwa shambulio hili limetekelezwa usiku wa kuamkia leo kwenye mji wa Liboi.

Taarifa ya msemaji wa polisi imesema kuwa, awali wapiganaji hao walivamia askari waliokuwa lindo lakini wakazidiwa na kisha walienda kujikusanya na kurejea wakiwa kwenye idadi kubwa na kuanza kuwashambulia tena.

Polisi mmoja aliyejeruhiwa kwenye makabiliano hayo, amesafirishwa kupelekwa kwenye hospitali kuu ya Nairobi kwa matibabu zaidi, huku wengine watatu waliojeruhiwa wanaendelea kupatiwa matibabu jirani na hospitali iliyo kwenye kambi ya Dadaab.

Kundi la Al-Shabab la nchini Somalia lenye uhusiano na mtandao wa kigaidi duniani la Al-Qaeda, limekiri kuhusika kwenye shambulizi hilo, ambalo limetekelezwa sambamba kuelekea maadhimisho ya shambulizi la Westgate, ambalo watu 67 waliuawa.

Kwenye taarifa yake kundi hilo limedai kuwaua askari sita wa Kenya pamoja na kufanikiwa kupora silaha na magari na kuwateka askari wengine wawili.

Taarifa za kutekwa kwa askari hao zimethibitishwa pia na msemaji wa jeshi la Polisi, ambaye amesema kuwa, Polisi wote waliokuwa doria walipatikana isipokuwa askari wawili tu ambao hawajulikani walipo.

Kundi la Al-Shabab linapambana kutaka kuuangusha utawala wa Mogadishu unaotambuliwa na Jumuiya ya Kimataifa, lakini pia limekuwa likitekeleza mashambulizi dhidi ya Serikali ya Kenya, ambapo tukio la mwisho walilitekeleza kwenye chuo kikuu cha Garisa ambapo watu 148 waliuawa wengi wakiwa wanafunzi.