DRC-TANZANIA

Rais Joseph Kabila ziarani nchini Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila Kabange anafanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini Tanzania kuanzia Jumatatu hii. Amewasili katika mji mkuu wa Tanzania, Dar es Salaam Jumatatu hii, na amepokelewa na mwenyeji wake John Pombe Magufuli.

Joseph Kabila, rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Februari 3, 2015.
Joseph Kabila, rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Februari 3, 2015. © AFP PHOTO / CARL DE SOUZA
Matangazo ya kibiashara

Alipowasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa Julius Nyerere, Rais Kabila amepokelewa na viongozi mbalimbali wa nchi hiyo akiwemo rais John Magufuli na maafisa wengine wa serikali.

Rais Joseph Kabila amepokea heshima ya kupigiwa mizinga 21 katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa ajili yake na baadaye kushuhudia burudani ya vikundi vya ngoma.

Katika ziara yake Rais Kabila anatarajia pia kuzungumzia masuala ya kisiasa nchini mwake ambapo uchaguzi uliopangwa kufanyika Novemba mwaka huu umesogezwa mbele mpaka mwakani jambo ambalo limeleta hali ya wasiwasi kwa wananchi wa DR Congo.

Jumanne hii Joseph Kabila Kabange atakutana kwa mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais John Pombe Magufuli. Baada ya mazungumzo hayo, Rais Kabange ataweka jiwe la msingi la jengo la mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA) na baadaye kushiriki dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na mwenyeji wake Rais John Pombe Magufuli katika Ikulu Jijini Dar es Salaam.