TANZANIA-DRC

Biashara, usalama na uchaguzi kuwa sehemu ya mazungumzo kati ya Rais wa Tanzania na DRC

Rais wa Tanzania, John Magufuli akiwa na mgeni wake rais wa DRC, Josephu Kabila wakati alipowasili jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Rais wa Tanzania, John Magufuli akiwa na mgeni wake rais wa DRC, Josephu Kabila wakati alipowasili jijini Dar es Salaam, Tanzania. Ikulu/Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Josephu Kabila Kabange, yuko nchini Tanzania na kulakiwa na mwenyeji wake rais John Pombe Magufuli, pamoja na makamu wa rais wa Tanzania, Samia Suluhu, ambapo atakuwa nchini humo kwa ziara ya kikazi ya siku tatu, imesema taarifa ya Ikulu ya Dar es Salaam.

Matangazo ya kibiashara

Baada ya kutua na ndege ya Serikali katika uwanja wa kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere, rais Kabila alipigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride lililoandaliwa kwaajili yake.

Hii leo rais Kabila atakuwa na mazungumzo na rais Magufuli kwenye Ikulu ya dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine watazungumzia kuhusu uhusiano wa nchi hizo mbili, kiuchumi pamoja na usalama, ambapo baadae ataweka jiwe la msingi katika jengo la mamlaka ya Bandari jijini Dar es Salaam.

Ziara ya rais Kabila nchini Tanzania, imekuja wakati huu nchini mwake mazungumzo ya kitaifa kusaka suluhu ya kisiasa yakiahirishwa kwa mara nyingine hapo jana kutokana na kutotimia kwa akidi ya wajumbe wanaoshiriki.

Wadadisi wa mambo wanasema kuwa suala la usalama mashariki mwa DRC ambako nchi ya Tanzania ina wanajeshi wake, ni suala ambalo viongozi hawa watalizungumzia bila kuweka kando suala la uchaguzi wa nchi hiyo, ambapo nchi ya Tanzania inaelezwa kuwa mfano wa kupigania amani na usalama wa nchi za ukanda.