KENYA-AU

Kenya yampendekeza balozi Amina Mohammed kuwania kiti cha uenyekiti wa AU

Balozi wa Amina Mohammed, ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje wa Kenya, aliyependekezwa na Rais Uhuru Kenyatta, kuwania kiti cha uenyekiti wa AU.
Balozi wa Amina Mohammed, ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje wa Kenya, aliyependekezwa na Rais Uhuru Kenyatta, kuwania kiti cha uenyekiti wa AU. UN Photo/JC McIlwaine

Nchi ya Kenya imewasilisha jina la waziri wake wa mambo ya kigeni na biashara za kimataifa, Amina Mohammed, kuwania nafasi ya mwenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika.

Matangazo ya kibiashara

Mwezi January mwaka huu, umoja wa Afrika uliahirisha uchaguzi wa mkuu mpya wa tume hiyo kuchukua nafasi ya Nkosozana Dlamini-Zuma ambaye ametangaza rasmi kutowania nafasi hiyo kwa muhula wa pili.

Katika mkutano wa mwisho wa wakuu wa nchi za umoja wa Afrika uliofanyika jijini Kigali, Rwanda, nchi wanachama zilishindwa kumchagua mkuu mpya wa tume hiyo baada ya kushindwa kufikia robo tatu ya kura zilizokuwa zikihitajika kwa waliokuwa wakiwania nafaso hiyo.

Bado haijafahamika ikiwa balozi Amina Mohammed ndiye atakuwa chaguo la nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika mashariki au la, kwa kuwa mgombea wa Uganda na aliyewahi kuwa makamu wa rais Specioza Kazibwe bado yuko kwenye mbio za kuwania kiti hicho.

Balozi Amina Mohammed aliteuliwa kushika nafasi ya waziri wa mambo ya nje nchini Kenya mwaka 2013 na kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo kwenye ukanda wa Afrika Mashariki, na sasa wachambuzi wa mambo wanampa nafasi ya kuziba nafasi ya Dlamini-Zuma.

Wagombea wengine kwenye nafasi hiyo ni pamoja na mgombea kutoka Equatorial Guinea Agapito Mba na kutoka Botswana Vensom Moitoi, wagombea wote hawa majina yao yatawasilishwa October 14 kuelekea uchaguzi wa mwezi January mwakani.