BURUNDI-UCHUMI

Shule zaathirika kutokana na mgogoro unaoendelea Burundi

Hali ya nchi yaathiri shule nyingi za umma sawa na zile za binafsi nchini Burundi.
Hali ya nchi yaathiri shule nyingi za umma sawa na zile za binafsi nchini Burundi. RFI/Sonia Rolley

Wiki mbili baada ya mwaka wa shule kuanza nchini Burundi, hazina za shule nyingi nchini humo ni tupu na athari zimekua zikijitokeza kwa wanafunzi wa shule za binafsi sawa na zile za umma.

Matangazo ya kibiashara

Nchini Burundi shule za serikali na shule zenye mabweni zinakabiliwa na matatizo makubwa ya kiufundi na kifedha. Inaarifiwa kuwa tayari kunaripotiwa ukosefu wa fedha na vifaa, huku shule nyingi zenye mabweni pia zikiwa zinadaiwa mzigo wa pesa za chakula.

Hata hivyo, mabweni mengi hayana magodoro kwa ajili ya malazi kwa wanafunzi. Mashirika ya kiraia na wizara ya elimu wanasema kutiwa wasiwasi na hali hii.

Wizara ya Elimu kwa upande wake inabaini kwamba licha ya nia yake ya kufanya vizuri, ina uwezo mdogo wa kifedha ili kukidhi mahitaji yake yote.

Hali hii inajiri wakati ambapo uchumi wa burundi umeendelea kudorora huku mfumko wa bei ukiendelea kushuhudiwa nchini kote.

Kwa sasa noti za faranga mia moja zimekua haba nchini na hali hii inasumbua sana wafanyabiashara pamoja na wateja wao.

Burundi imeanza kushuhudia hali hii baada ya nchi za magharibi kuchukua uamuzi wa kusimamisha msaada wake kwa Burundi. Serikali ya Burundi imekua ikitegemea Urusi na China lakini ni wazi kwamba nchi hizi hazisaidii chochote.

Wadadisi wanasema Burundi haiwezi kujikwamua kiuchumi kutokana na kwamba haina rasilimali za kutosha, na nchi kama Urusi na China ingawa zinatoa msaada kwa Burundi, lakini hautoshi.

Kabla ya nchi za magharibi kuchukua uamuzi wa kusitisha msaada wake kwa Burundi nchi hii ilikua ikitegemea 51% ya msaada kutoka nje.