AFRIKA KUSINI-KENYA

Zuma ziarani nchini Kenya, ulinzi, biashara na uwekezaji ndio ajenda ya mazungumzo na Rais Kenyatta

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma REUTERS/Mike Hutchings

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu nchini Kenya, kuanzia Jumatatu ya tarehe 10 October hadi tarehe 12 ya mwezi October mwaka huu, ikiwa ni ziara ya kwanza kufanywa na kiongozi wa taifa hilo toka kumalizika utawala wa kibaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

Matangazo ya kibiashara

Ziara hii inalenga kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili katika masuala ya uchumi, siasa, utamaduni na huduma za kijamii na taifa la Kenya, taifa linalotajwa kuwa na uchumi imara kwenye jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki.

Ziara ya rais Zuma itatoa fursa kwa nchi hizi mbili kupitia upya hatua zilizopigwa kwenye maeneo muhimu ya ushirikiano, maeneo ambayo pamoja na mambo mengine, yanahusu: biashara na uwekezaji; kilimo; utalii na maendeleo na miundo mbinu.

Rais Jacob Zuma na mwenzake wa Kenya, Uhuru Kenyatta watabadilishana mawazo kuhusu umuhimu wa ushirikiano wa kikanda, bara na kidunia.

Nchi ya Kenya ni miongoni mwa mataifa ambayo ni washirika muhimu na taifa la Afrika Kusini kwenye masuala ya ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji, ambapo Afrika Kusini ni taifa la nne lenye uwekezaji mkubwa nchini Kenya, ambapo inasafirisha bidhaa nchini humo zinazofikia thamani ya Randi bilioni 8.3 na kuingiza bidhaa kutoka Kenya zenye thamani ya Randi za Afrika Kusini milioni 366 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015.

Hivi sasa zaidi ya makumpuno 60 ya Afrika Kusini yanafanya shughuli zao nchini Kenya na Afrika Kusini ndio taifa la 6 kiuwekezaji nchini Kenya, baada ya China, Uingereza, Marekani, India na Nigeria na pia ndio taifa kubwa linalofanya biashara zaidi na Kenya nje ya nchi za ukanda wa SADC.

Nchi hizi mbili zinatarajiwa kutiliana saini makubaliano kadhaa ya maelewano (MOU) katika maeneo ya ulinzi, Polisi, mambo ya ndano, mazingira; Mapato; maendeleo ya miundombinu chini ya mkataba wa eneo la kiuchumi la Lamu-Sudan Kusini-Ethiopia.

Kutiwa saini kwa makubaliano haya kunaendelea kudhihirisha dhamira ya wazi na kweli ya Afrika Kusini katika kuimarisha uhusiano wake na taifa la Kenya.

Rais Zuma anawasili nchini Kenya baada ya kumaliza mahojiano yake na mkurugenzi wa ofisi ya mkaguzi wa mali ya uma Thuli Madonsela, ambaye anamchunguza dhidi ya tuhuma za kuwa na uhusiano na familia tajiri yenye asili ya Kihindi, inayodaiwa kuwa inaushawishi juu yake kuhusu uteuzi wa mawaziri kadhaa kwenye Serikali yake.