SUDANI KUSINI-UN

Urusi yasisitiza hakuna haja ya Sudan Kusini kuwekewa vikwazo vya silaha

Petr V. Iliichev, naibu balozi wa Urusi kwenye umoja wa Mataifa.
Petr V. Iliichev, naibu balozi wa Urusi kwenye umoja wa Mataifa. UN Photo/Manuel Elias

Nchi ya Urusi inasema kuwa hakuna haja ya taifa la Sudan Kusini kuwekewa vikwazo vya silaha licha ya ripoti ya katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon kudai kuwa utawala wa Juba, umefanya kidogo sana kuruhusu walinda amani zaidi kupelekwa nchini humo pamoja na kutoa uhuru wa kufanya doria kwa wanajeshi ambao wako tayari nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Mwezi uliopita rais Salva Kiir alikubali kupelekwa kwa wanajeshi elfu 4 wa ziada pamoja na kuruhusu wanajeshi elfu 12 ambao wako tayari nchini humo kufanya doria kwa uhuru kwa lengo la kuwalinda raia.

Rais Kiir alikubali pendekezo hilo baada ya ziara ya wajumbe wa baraza la usalama la umoja wa Mataifa ambao walienda nchini humo kujionea hali ilivyo na kuitaka Serikali ya Juba kuruhusu nyongeza zaidi ya wanajeshi.

Katika azimio la mwezi Agosti mwaka huu, baada ya kuzuka kwa makabiliano ya mwezi Julai mjini Juba, wajumbe wa nchi 15 wanachama wa baraza la usalama, walitishia kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya silaha ndani ya siku tano baada ya kupokea ripoti ya katibu mkuu iliyodai kuwa utawala wa Juba hauoneshi ushirikiano.

Naibu balozi wa Urusi kwenye umoja wa Mataifa, Petr Iliichev, amesema kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa, tathimini ya ripoti ya katibu mkuu Ban Ki Moon, haioneshi ikiwa utawala wa Juba unazuia utekelezwaji wa maazimio ya baraza la usalama.

“Msimamo wetu kupinga nchi hiyo kuwekewa vikwazo vya silaha uko palepale na haubadiliki. Jana tulikuwa tukijadili kuhusu Jamhuri ya Afrika ya Kati ambako vikwazo vya silaha vimewekwa lakini hakuna taarifa rasmi ya utekelezaji.” alisema balizi huyo.

Hata hivyo balozi wa Uingereza kwenye umoja wa Mataifa, Matthew Rycroft, amesema kuwa kwa upande wake atazungumza na wajumbe wengine kuamua ikiwa washinikize au la kuwekewa vikwazo kwa nchi hiyo.

Kwa upande wake naibu balozi wa Marekani kwenye umoja wa Mataifa, David Pressman, amesema kuwa wanatarajia kuwa na mazungumzo ya kina kuhusu suala hilo na kwamba wataamua baadae hatua za kuchukua.