BURUNDI-ICC

Burundi yajiondoa rasmi katika ICC

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza, atia saini sheria iliopitishwa na bunge pamoja na seneti ya kuiondoa Burundi katika mkataba wa Roma unaosimamia mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu wa kivita ICC.
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza, atia saini sheria iliopitishwa na bunge pamoja na seneti ya kuiondoa Burundi katika mkataba wa Roma unaosimamia mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu wa kivita ICC. © RFI-KISWAHILI

Nchi ya Burundi hatimaye imejiondoa rasmi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutia saini sheria iliopitishwa na bunge pamoja na seneti ya kuiondoa Burundi katika mkataba wa Roma unaosimamia mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu wa kivita ICC.

Matangazo ya kibiashara

Burundi imekua nchi ya kwanza kujiondoa katika Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC.
Tayari mahakama ya ICC imeitaja mipango ya Burundi ya kujiondoa katika mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu wa kivita ICC kuwa 'pigo' katika vita dhidi ya watu wasioheshimu sheria.

Mwendesha mashtaka wa ICC Fatou Bensouda ameendelea kutsisitiza kuwa uamuzi wa Burundi wa kujiondoa ICC si mwisho wa kutofunguliwa mashitaka
Mwendesha mashtaka wa ICC amesema kuwa atachunguza kile kilichotokea Burundi wakati wa maandamano dhidi ya rais Pierre Nkurunziza

Aliyekuwa waziri wa haki nchini Senegal Sidiki Kaba,ambaye anaongoza bodi hiyo ya ICC ,alitoa wito kwa Burundi kuzungumzia wasiwasi wake badala ya kujiondoa katika mahakama hiyo.

Kimsingi, Mahakama ya Kimataifa haiwezi tena kuchunguza kwa jitihada zake nchini Burundi, mara tu mwaka mmoja utakua umemalizika baada ya nakala hiyo kutiliwa saini na rais wa Burundi. Hata hivyo uamuzi huo hautoitenga Burundi kutofuatiliwa na mahakama ya kimataifa. Inatosha tu kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuruhusu nchi hiyo kufuatiliwa na mahakama ya kimataifa kama ilivyokuwa kwa kesi ya Darfur mwaka 2005 na Libya mwaka 2011.

Jumuiya ya kimataifa pia imeweka wazi kesi ya wanachama ambao wataamua kujiondoa katika ICC ili kuepuka mashtaka, mtaalamu aliyehojiwa na RFI ameeleza. Sheria za Roma zinaeleza kwamba 'uamuzi wa kujiondoa ICC unachukua mwaka mmoja baada ya tarehe ambayo uamuzi huo utakua umewasilishwa kwa vyombo husika,' uamuzi wa kujiondoa hautakua na athari kwa kesi ambazo tayari zinaendelea kushughulikia na taasisi hiyo ya kimataifa hata kama uamuzi huo utasahihishwa.

Mwendesha mashitaka wa ICC, Fatou Bensouda, alizindua mwezi April mwaka huu uchunguzi wa awali kuhusu mauaji, mateso na ubakaji nchini Burundi. Wakati huo huo, kundi la wanasheria liliwasilisha kwa Mahakam ya Kimataifa ya Jinai (ICC) tangu miezi mitatu iliyopita kesi ya waathirika zaidi ya mia moja au warithi wa waathirika wa unyanyasaji huo.

Hatimaye, na hii pengine ni moja ya sababu iliyopelekea serikali ya Burundi kuchukua uamuzi wa kujiondoa katika ICC: baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa liliamua, siku chache tu zilizopita kuunda tume ya uchunguzi wa kimataifa kufuatia ripoti ya wataalam iliyohusisha serikali ya Burundi katika uhalifu mkubwa. Orodha ya wahusika katika uhalifu huo tayari imewekwa wazi.

Barua iliotiwa saini na rais Nkurunziza kuiondoa Burundi katika ICC.