Mashirika 10 yapigwa marufuku kuendesha shughuli zao nchini Burundi
Serikali ya Burundi imepiga marufuku mashirika 10 ya kutetea haki za binadamu kuendesha shughuli zao katika ardhi ya Burundi. Hatua hiyo imechukuliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Pascal Barandagiye.
Imechapishwa:
Serikali ya Burundi inasema mashirika hayo yamekua yakichochea chuki na uhasama baina ya raia wa Burundi waishio ndani na nje ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi hatua hii imechukuliwa kwa minajili ya kupambana na ghasia.
Muungano wa vyama vinavyotetea haki na maslahi ya waandishi habari (UBJ) na shirika la haki za binadamu na za wafungwa (APRODH) ni miongoni mwa mashirika yaliyopigwa marufuku kuendesha shughuli zao katika ardhi ya Burundi.
Itafahamika kwamba Mashirika matano ya kutetea haki za binadamu yamevunjwa kabisa, likiwemo lile la APRODH linaloongozwa na mwanaharakati Pierre-Claver Mbonimpa, ambaye yuko uhamishoni barani Ulaya, baada ya kunusurika kifo aliposhambuliwa na watu wasiojulikana mwaka jana alipokua akielekea nyumbani kwake katika kata ya Carama, mtaani Kinama, kaskazini mwa mji wa Bujumbura.
Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Ndani amesema mashirika kama vile Iteka, SOS-Torture pamoja na UBJ, yamesimamishwa kwa muda.