MOROCCO-TANZANIA

Tanzania na Morocco zatiliana saini mikataba 21 ya ushirikiano wa kiuchumi na biashara

Nchi ya Tanzania na Morocco zimetiliana saini mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo zaidi ya 21, mikataba ambayo itashuhudia nchi hizi mbili zikiimarisha uhusiano wao ambao toka nchi ya Morocco ijitoe kwenye umoja wa Afrika haukuwa mzuri sana na nchi za Afrika.

Mfalme wa sita wa Morocco, Mohamed akiwa na mwenyeji wake Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, Ikulu, Dar es Salaam, 24 October 2016.
Mfalme wa sita wa Morocco, Mohamed akiwa na mwenyeji wake Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, Ikulu, Dar es Salaam, 24 October 2016. Ikulu/Tanzania/issa Michuzi
Matangazo ya kibiashara

Nchi hiyo ilijitoa miaka 30 iliyopita, ambapo wakati huo rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere, alikuwa mwenyekiti wa iliyokuwa Jumuiya ya nchi huru za Afrika OAU, ambapo alihusika katika kujaribu kupatanisha nchi hiyo na eneo la Sahara Magharibi linalojitenga na nchi hiyo.

Mfalme wa 6 wa Morocco alifanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, kwenye ikulu ya jijini Dar es Salaam, ambapo walizungumzia uhusiano wa nchi hizo mbili na kukubaliana kuanzishwa kwa jukwaa la kisiasa kati ya nchi hizi mbili.

Jukwa hili lina lengo la kujaribu kurejesha uhusiano wa kisiasa baina ya nchi hizo mbili ambao haukuwepo toka taifa hilo lilipotangaza kujitenga kutoka kwenye umoja wa Afrika.

Mbali na kukubaliana kurejesha jukwaa la kisiasa baina ya nchi hizi mbili, viongozi hawa wamekubaliana pia kushirikiana kwenye sekta ya usalama, ambapo wamekubali kubadilishana ujuzi na taarifa za kiintelijensia.

Mfalme wa 6 wa Morocco (kushoto) akiwa na mwenyeji wake Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli (kulia). 23 October 2016.
Mfalme wa 6 wa Morocco (kushoto) akiwa na mwenyeji wake Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli (kulia). 23 October 2016. Ikulu/Tanzania/Issa Michuzi

Katika sekta ya kiuchumi, wakuu hawa wa nchi wamekubaliana kuimarisha biashara baina ya nchi hizi mbili, hasa katika bidhaa za kilimo, pamoja na kutafuta maeneo zaidi ya uwekezaji ambayo yatazinufaisha nchi zote mbili.

Mikataba mingine iliyotiwa saini ni pamoja na ushirikiano katika sekta ya Uvuvi, Viwanda, Madini, Mbolea, masuala ya bima, Uwekezaji, reli, biashara, elimu na afya, huku maeneo yote haya, nchi hizi mbili zikikubaliana kubadilishana wataalamu na kuwezeshana kufikia maelengo endelevu.

Kwa upande wake Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, alipongeza ziara ya mfalme Mohamed wa 6 nchini mwake, ambapo ni ziara ya kwanza kufanywa na kiongozi wa taifa hilo nchini humo pamoja na kwenye nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.

Wataalamu wa mambo wanasema ziara hii ya mfalme wa 6 wa Morocco imelenga kujaribu kuzishawishi nchi za Afrika kuikubali na kuirejesha kwenye umoja wa Afrika, juhudi ambazo wengi wanasema huenda ikawezekana, na wengine wakidai kuwa suala la kijitenga kwa eneo la Sahara Magharibi itakuwa kikwazo.