SUDANI KUSINI-UGANDA-WAASI

Waasi wa Sudani Kusini wadai kitita cha fedha kuwaachia mateka raia wa Uganda

Kundi linalosadikiwa kuwa ni waasi wa nchini Sudan Kusini, limetaka kulipwa kitita kikubwa cha pesa kwa kubadilishana na raia wa Uganda waliotekwa nyara, wakati basi lao liliposhambuliwa na waasi hao kwenye barabara ya Nimule-Juba.

Kiongozi wa waasi wa Sudani Kusini, Riek Machar, ambaye wapiganaji wake wanadaiwa kutekeleza vitendo vya utekaji nyara, picha ya tarehe 29 April 2014.
Kiongozi wa waasi wa Sudani Kusini, Riek Machar, ambaye wapiganaji wake wanadaiwa kutekeleza vitendo vya utekaji nyara, picha ya tarehe 29 April 2014. AFP Photo:UNMISS/Isaac Alebe Avoro
Matangazo ya kibiashara

Taarifa iliyotolewa na mkuu wa jeshi la Polisi nchini Sudan Kusini, Jenerali Makur Muruol, imethibitisha kuwa wamepokea madai ya waasi hao.

Mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu, jumla ya raia wa Uganda 41 wameripotiwa kutekwa nyara na kundi la waasi wanaoaminika kuwa ni watiifu kwa aliyekuwa makamu wa rais wa taifa hilo Riek Machar.

Raia hao wanaelezwa kuwa walitekwa nyara wakati wakiwa kwenye mabasi wakisafiri kwenye eneo la mpaka wa nchi hiyo na Sudan Kusini.

Miongoni mwa mateka hao, 23 wanaripotiwa kuwa walitekwa nyara katika barabara ya Nimule-Juba mwezi May mwaka huu, na wafanyabiashara wengine wa mbao ambao wako 8 walitekwa mwezi Julai mwaka huu kaskazini mwa nchi ya Uganda kwenye wilaya ya Lamwo.

Mkimbizi akiandamana na askari wa kulinda amani, karibu na kambi ya kulinda raia (POC) ya Umoja wa Mataifa mjini Juba, Oktoba 4, 2016.
Mkimbizi akiandamana na askari wa kulinda amani, karibu na kambi ya kulinda raia (POC) ya Umoja wa Mataifa mjini Juba, Oktoba 4, 2016. ALBERT GONZALEZ FARRAN / AFP

Wakati mateka wengine 8 wakiachiwa baada ya kulipwa kwa dola za Marekani milioni 3 kwa kila mtu, mateka wengine wanne ambao ni wafanyabiashara wakatekwa ndani ya mwezo huo huo.

Wafanyabiashara hao ambao mpaka sasa hawajulikani walipo, wanadaiwa kuwa walitekwa nyara na wapiganaji waasi wa Pajok katika kaunti ya Magwii magharibi mwa jimbo la Equatoria nchini Sudan Kusini.

Ni raia sita tu ndio wanaoelezwa kuwa walifanikiwa kuwatoroka mateka wao, na kupatikana na jeshi la Polisi la Sudan Kusini kabla ya kukabidhiwa kwa Serikali ya Uganda.

Waasi wa nchini Sudan Kusini wamekuwa wakituhumiwa na Serikali ya Juba kwa kuendesha vitendo vya kihalifu dhidi ya raia, tuhuma ambazo kiongozi wa waasi Riek Machar amekanusha jeshi lake kuhusika.

Biashara kati ya nchi ya Uganda na Sudan Kusini imeendelea kuathirika kutokana na kukithiri kwa vitendo vya utekaji nyara vinavyodaiwa kufanywa na makundi ya waasi kwenye nchi hiyo.