KENYA-ADHABU YA KIFO

Rais Kenyatta awafutia adhabu ya kifo wafungwa zaidi ya elfu 2

Nchini jumla ya wafungwa elfu 2 na 747 waliokuwa wamehukumiwa adhabu ya kifo na mahakama, wamepata ahueni, baada ya Rais Uhuru Kenyatta, kutengua hukumu ya wafungwa hao kunyongwa na kuagiza wafungwe maisha.

Moja ya matangazo ya shirika la Amnesty International kuhusu adhabu ya kifo
Moja ya matangazo ya shirika la Amnesty International kuhusu adhabu ya kifo Amnesty International
Matangazo ya kibiashara

Katika tangazo hili la Rais lilitolewa Jumatatu ya tarehe 24 October, rais Kenyatta, ameagiza watu waliokuwa tayari kunyongwa, watumikie adhabu ya kufungo cha maisha jela.

Nchini Kenya, adhabu ya kifungo cha maisha ina maanisha kuwa mshtakiwa atakaa jela maisha yake yote labda itokee kwa rais kutoa msamaha.

Taarifa ya ikulu imesema kuwa, Rais ameahirisha adhabu ya kifo kwa wafungwa elfu 2655 wanaume na wanawake 92, ambao sasa wataondolewa kwenye orodha ya kunyongwa na badala yake watatumikia kifungo cha maisha jela.

Mwaka 2009, rais wa zamani wa taifa hilo, Mwai Kibaki, aliagiza kuondolewa adhabu ya kifo kwa wafungwa wote waliohukumiwa adhabu hiyo na badala yake watumikie kifungo cha maisha jela.

Uamuzi huu utawagusa zaidi ya wafungwa elfu 4 na wakati huo huo uamuzi huu unaelezwa kuwa ndio idadi kubwa zaidi ya wafungwa kuwahi kuondolewa adhabu ya kifo.

Kwa mujibu wa sheria ya magereza ya Kenya, adhabu ya kifo, hutekelezwa kwa mtuhumiwa kunyongwa kwa kamba.

Mara ya mwisho kutekelezwa kwa adhabu ya kunyongwa nchini Kenya ilikuwa mwaka 1987, baada ya watuhumiwa wa jaribio la mapinduzi la mwaka 1982 kuhukumiwa adhabu ya kifo.

Licha ya kuwa adhabu ya kunyongwa haijatekelezwa toka wakati huo, mamia ya watu wamehukumiwa adhabu ya kifo kila mwaka.

Rais Kenyatta pia kwa kutumia madaraka yake chini ya katiba ya Kenya, alitia saini kuachiliwa huru kwa wafungwa 102 ambao wametumikia adhabu zao jela kwa muda mrefu zaidi.

Uamuzi huu wa rais Kenyatta umekuja saa chache tu baada ya wananchi wa Kenya kuelekea kumaliza mjadala kuhusu utekelezwaji wa adhabu ya kifo nchini humo.

Kwa mujibu wa sheria za Kenya, kuna aina tano za makosa ambayo mtu huweza kuhukumiwa kifo, makosa hayo yanahusu: mauaji, uhaini, wizi wa kutumia mabavu, jaribio la wizi na kufanya vurugu na kuapa kwa lengo la kutaka kutekeleza uhalifu.

Uamuzi huu umeonekana kupongezwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Kenya ambayo yamekuwa mstari wa mbele kupinga kutekelezwa kwa adhabu ya kifo.