TANZANIA-KENYA

Wakuu wa nchi ya Kenya na Tanzania wakubaliana kuimarisha uhusiano wao

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta (kushoto) akiwa na mgeni wake Rais wa Tanzania, John Magufuli (kulia), 30 October 2016
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta (kushoto) akiwa na mgeni wake Rais wa Tanzania, John Magufuli (kulia), 30 October 2016 Kenya State House/ Media handouts

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, ameanza ziara ya siku mbili nchini Kenya, ambapo amekutana kwa mazungumzo na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta, ambapo wakuu hawa wa nchi wametiliana saini makubaliano kadhaa ya ushirikiano.

Matangazo ya kibiashara

Wakizungumza na wanahabari baada ya kumaliza mazungumzo yao ya faragha kwenye ikulu ya Nairobi, viongozi hao wamekubaliana kuendelea kuimarisha uhusiano uliopo baina ya nchi hizo na kufanyia kazi changamoto zilizopo.

Rais Magufuli amesema amemuhakikishia Rais Kenyatta kuendelea kushirikiana nae katika masuala ya maendeleo na kwamba kama ndugu hakuna suala ambalo watashindwa kulipatia ufumbuzi.

Kwa upande wake Rais Kenyatta, amesema kuwa, pamoja na kuwa kuna masuala ambayo viongozi hao hawakuweza kuyapatia ufumbuzi kwenye mazungumzo yao, jitihada zinaendelea ili kupata muafaka.

Viongozi hawa wawili pia wamewaagiza mawaziri wao wa mambo ya nje, Amina Mohamed wa Kenya na Augustin Mahiga wa Tanzania, wakutane mwishoni mwa mwaka huu kuzungumzia masuala ambayo yamesalia na yanahitaji kupatiwa ufumbuzi.

Miongoni mwa masuala ambayo watu wengi walitarajia kuona viongozi hawa wakiyaweka wazi kwenye mkutano wao na waandishi wa habari, hayakuwekwa wazi kama ilivyotarajiwa jambo ambalo limeendelea kuibusha maswali kuhusu maeneo kadhaa ambayo nchi hizi zinavutana.

Itakumbukwa kuwa suala la watalii kuingia nchini Tanzania lilikuwa ni suala lililoibusha sintofahamu kubwa mwaka jana na hadi sasa, huku pia uhuru wa raia wa Kenya kuingia Tanzania bila kubugudiwa ni suala jingine ambalo halikuzungumzwa na viongozi hawa

Hata hivyo katika kutuliza sintofahamu hii, viongozi hawa wamewahakikishia raia wao kutokuwa na hofu, na kwamba tayari masuala kadhaa yameanza kupatiwa ufumbuzi na makubaliano yake yatatangazwa hivi karibu.

Rais Magufuli pia akasifia namna ambavyo amefanikiwa kupunguza suala la ukiritimba na rushwa Serikali, jambo ambalo amemuomba Rais Kenyatta kulishughulikia ipasavyo kwakuwa linakwamisha maendelo ya nchi.