RWANDA-UFARANSA-MAUAJI

Rwanda: maofisa waandamizi 22 wa Ufaransa walihusika katika mauaji ya kimbari

Rais wa Rwanda Paul Kagame akiwasha moto wa kumbukumbu katika eneo la kumbukumbu la mauaji ya kimbari mjini Kigali, wakati wa maadhimisho ya miaka 21 ya mauaji ya kimbari, Aprili 7, 2015.
Rais wa Rwanda Paul Kagame akiwasha moto wa kumbukumbu katika eneo la kumbukumbu la mauaji ya kimbari mjini Kigali, wakati wa maadhimisho ya miaka 21 ya mauaji ya kimbari, Aprili 7, 2015. AFP/Stéphanie Aglietti

Tume ya Kitaifa dhidi ya Mauaji ya Kimbari nchini Rwanda imetoa orodha ya maafisa waandamizi 22 wa Ufaransa ambao inawatuhumu kuhusika katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, katika kukabiliana na uamuzi wa majaji wawili wa Ufaransa wanaoendesha upya uchunguzi katika shambulio dhidi ya ndege ya Rais wa zamani Juvenal Habyarimana.

Matangazo ya kibiashara

"Maafisa wa ngazi ya juu wa Ufaransa na wanasiasa walitekeleza uhalifu mbaya nchini Rwanda," Tume ya Kitaifa dhidi ya Mauaji ya Kimbari (CNLG) imeshtumu katika nakala iliyowasilishwa Jumanne kwenye ofisi za shirika la habari la AFP. Nakala hii inayojulikana kama "njama ya kesi ya ndege ya Habyarimana, Ufaransa yahusika katika mauaji hayo. "

Rwanda inaishtumu kwa miaka kadhaa Ufaransa kushiriki katika mauaji ya kimbari, ambapo watu zaidi ya 800,000, wengi wao wakiwa kutoka jamii ya Watutsi waliuawa. Shambulizi la Aprili 6, 1994 dhidi ya ndege ya rais, ambapo aliuawa rais kutoka jamii ya Wahutu Juvenal Habyarimana na mwenzake wa Burundi Cyprien Ntaryamira, linachukuliwa kama tukio lililozua mauaji ya kimbari.

Lakini uhusiano kati ya nchi hizi mbili uliingia upya matatani tangu mahakama ya Ufaransa kuanzisha uchunguzi kwa kusikia ushuhuda wa mkuu wa zamani wa majeshi ya Rwanda, Kayumba Nyamwasa, ambaye anamtuhumu Rais wa sasa wa Rwanda, Paul Kagame, kwamba ndiye mwanzilishi wa shambulizi dhidi ya rais Juvenal Habyarimana.

Kwa mujibu Tume ya Kitaifa ya Kupambana dhidi ya Mauaji ya Kimbari (CNLG), uamuzi wa hivi karibuni wa Uifaransa kuanzisha upya uchunguzi kuhusu shambulio dhidi ya ndege ya rais Juvenal Habyarimana Aprili 6, 1994 "inalenga kuficha" ukweli kuhusu kuhusika kwa Ufaransa katika mauaji ya kimbari nchini Rwanda. Tume hii imetoa orodha ya maafisa wandamizi 22 wa Ufaransa ambao wanatuhumiwa kula njama bali pia kwa kuhusika katika mauaji hayo. "Maafisa wa Ufaransa walihusika katika mauaji ya kimbari kama wahalifu na washirika," CNLG imebaini.

Jenerali Jacques Lanxade, aliyekuwa Mkuu wa majeshi ya Ufaransa, na jenerali Jean-Claude Lafourcade, ambaye alikua kiongozi wa kikosi kiliyojulikana kwa jina la Turquoise Juni 22, 1994 nchini Rwanda chini ya mamlaka ya Umoja wa Mataifa ni miongoni mwa maafisa hao waandamizi 22 wanaotajwa kuwa walihusika katika mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994.

Nchini Rwanda, kamati ya uchunguzi ilibaini kwamba shambulizi dhidi ya ndege ya Rais Habyarimana lilitekelezwa na watu wenye msimamo mkali kutoka jamii ya Wahutu kutaka kumuangamiza rais ambaye waliona kuwa ni mwenye msimamo wa wastani.