KENYA-UN

Kenya yatangaza kuwaondoa askari wake katika kikosi cha UN nchini Sudan Kusini

Askari wa umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, wakipiga doria kwenye kambi yao, Julai 20, 2016.
Askari wa umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, wakipiga doria kwenye kambi yao, Julai 20, 2016. REUTERS/Stringer

Serikali ya Kenya imetangaza kuwaondoa askari wake katika kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS). Uamuzi huo unakuja siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kumfuta kazi kamanda wa kikosi hicho kutoka Kenya.

Matangazo ya kibiashara

Jumanne wiki hii Novemba 2, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon alimfuta kazi Kamanda wa kikosi cha kulinda amani nchini Sudan Kusini (UNMISS) Jenerali Johnson Ondieki.

Moon alisema amechukua hatua hiyo baada ya kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa kushindwa kuwalinda raia dhidi ya mapigano yaliyozuka mwezi Julai mwezi huu.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema wanajeshi wa umoja wa mataifa nchini Sudan Kusini walishindwa kuwasadia raia wa kawaida na wafanyikazi wa kutoa misaada.

Umoja wa Mataifa ulituma kikosi hicho mwaka 2011 kulinda amani nchini humo.

Umoja wa mataifa umekiri kuwa vikosi vyake vya kulinda Amani Sudani Kusini vimeshindwa kuwalinda raia katika mji mkuu wa Juba wakati wa mapigono baina ya pande mbili mwezi Julai mwaka huu, ambapo watu kadhaa waliuawa na maelfu wengine kulazimika kuyahama makazi yao.

Serikali ya Kenya imesema imesikitishwa mno na sababu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa, kuwa Kamanda huyo alishindwa kuzuaia kuuawa kwa raia wa kawaida baada ya kuzuka kwa vita jijini Juba miezi kadhaa iliyopita.

Wizara ya Mambo ya nje imesema wanajeshi hao wanatarajiwa kurudi nyumbani haraka iwezekanavyo.

Kenya ina wanajeshi 1,000 katika kikosi hicho cha wanajeshi 16,000 cha kulinda amani.