KENYA-MAANDAMANO

Polisi nchini Kenya watumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji

Waandamanaji nchini Kenya wakiwarushia mawe polisi na waandishi wa habari, waliokuwa wakiripoti maandamano ya kupinga vitendo vya rushwa, Nairobi, 3 Novemba, 2016.
Waandamanaji nchini Kenya wakiwarushia mawe polisi na waandishi wa habari, waliokuwa wakiripoti maandamano ya kupinga vitendo vya rushwa, Nairobi, 3 Novemba, 2016. REUTERS/Thomas Mukoya

Polisi nchini Kenya wamewakabili waandamanaji wanaopinga vitendo vya ufisadi nchini humo, ambapo wametumia gesi za kutoa machozi na kuwachapa fimbo kuwatawanya waandamanaji jijini Nairobi.

Matangazo ya kibiashara

Mamia ya raia walikusanyika kwenye jiji la Nairobi baada ya kutolewa ripoti kupitia vyombo vya habari vya ndani kuhusu tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi kwenye wizara ya afya nchini Kenya.

Waziri wa afya nchini humo tayari amekanusha madai dhidi yake.

Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta ambaye anatarajiwa kuomba kuwania kiti hicho kwa muhula mwingine kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, aliapa kupambana na masuala ya ufisadi ikiwa angechaguliwa.

Upinzani nchini humo unamtuhumu rais Kenyatta kwa kuwalinda mafisadi kwenye Serikali yake na kushindwa kudhibiti vitendo vya rushwa.

"Tuliiunga mkono Serikali hapo kabla, lakini imetuangusha. Watoto wankufa hospitalini kwasababu ya rushwa," alisema Beatrice Shiko, mmoja wa wanaharakati wanaopinga vitendo vya rushwa.

Suala la rushwa linaonekana kuwa kikwazo cha wawekezaji kwenda nchini Kenya na nchi za ukanda wa Afrika Mashariki, suala ambalo wadadisi wa mambo wanasema kuwa, wanatarajia kuwa litakuwa ni ajenda kuu ya kampeni za kuingia ikulu mwaka ujao.

Mara kadhaa nchi wafadhili wa Kenya walitishia kusitisha misaada kwa nchi hiyo, wakitaka Serikali kukemea Polisi ambao wanawapiga raia wanaofanya maandamano ya amani.