TANZANIA

Magufuli: Nchi ya Tanzania haifungamani na upande wowote, asifu utawala wake

Nchi ya Tanzania imesisitiza kuwa msimamo wake kuhusu eneo la Western Sahara uko pale pale na kwamba haujabadilika, kwa kuwa nchi hiyo haifungamani na upande wowote.

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, Dar es Salaam, Novemba 4, 2016.
Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, Dar es Salaam, Novemba 4, 2016. Screenshot/Azama TV
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari kwenye ikulu yake jijini Dar es Salaam, kuadhimisha mwaka mmoja toka aingie madarakani, Rais John Pombe Magufuli, amesema suala la Polisario linabaki pale pale kama ilivyokuwa msimamo wa muasisi wa taifa hili, Julius Nyerere.

Rais Magufuli amesema kuwa, ziara ya mfalme Mohamed wa 6 wa Morocco aliyoifanya nchini mwake, haimanishi kuwa msimamo wa Tanzania umebadilika kuhusu suala la Sahel, na kwamba Tanzania haibagui rafiki.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa, kutokana na sera aliyonayo ya uchumi wa viwanda na ushirikiano wa kimataifa, haijalishi kama nchi anayoshirikiana nayo wanatofautiana kuhusu baadhi ya mausala.

Rais Magufuli amezungumzia suala hili kutokana na ukweli kuwa nchi ya Morocco imeendelea kukalia eneo la Sahel Magharibi, eneo ambalo hata umoja wa Mataifa umeshalitangaza kuwa ni nchi huru lakini Morocco imeendelea kulikalia.

Kuhusu ushirikiano na nchi za ukanda katika kipindi chake cha mwaka mmoja, Rais Magufuli amesema kama mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na mwenyekiti wa kamati ya usalama ya SADC "Troica" ataendelea kusaka suluhu kwenye nchi zenye mzozo.

Rais Magufuli amesema kuwa suala la Burundi kwa sasa liko mahali pazuri ambapo amepongeza kazi inayofanywa na mratibu wa mazungumzo ya amani rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa.

Kuhusu Sudan Kusini, Rais Magufuli amesema kuwa suala la nchi hiyo bado anaendelea kulifanyia kazi na kwamba ndio maana waliamua kuruhusu Sudan Kusini kuwa mwanachama mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuendelea kuisaidia kupata Suluhu.

Kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rais Magufuli amesema kuwa tayari ametuma ujumbe wake kwenda nchini humo kuonana na viongozi wa Serikali na wanasiasa wa upinzani, kuangalia namna ambayo mzozo wa nchi hiyo unaweza kutatuliwa.

Kuhusu masuala mengine ya ndani ya nchi yake, Rais Magufuli mbali na kusifu namna ambavyo amefanikiwa kutimiza ahadi alizoahidi wakati wa kampeni, amekiri pia bado anakabiliwa na changamoto kubwa kuwa kuzitimiza katika kipindi cha miaka mitano.

Kuhusu muswada wa sheria wa vyombo vya habari, Rais Magufuli amesema kuwa, hawezi kuingilia mchakato ulioko bungeni hivi sasa, na kuongeza kuwa ikiwa bunge litapitisha muswada wa huduma za vyombo vya habari, basi atautia saini kabla ya kuanza tena kwa mchakato wa kufanyiwa Marekebishom kauli ambayo imeonekana kumaliza kabisa juhudi za waandishi wa habari kuomba muda usogezwe.