KENYA-SOMALIA

Kesi ya kuzuia kufungwa kwa kambi ya Daadab nchini Kenya yaanza kusikilizwa

Kambi ya wakimbizi ya Daadab kaskazini mwa nchi ya Kenya, inayohifadhi wakimbizi wa Somalia
Kambi ya wakimbizi ya Daadab kaskazini mwa nchi ya Kenya, inayohifadhi wakimbizi wa Somalia UNHCR - kenya

Mahakama Kuu jijini Nairobi nchini Kenya, imeanza kusikiliza kesi iliyowasilishwa na Wanaharakati wa haki za binadamu, Mashirika ya kiraia na Shirika la Kimataifa la kutetea haki za Binadamu la Amnesty International kupinga mpango wa serikali kufunga kambi ya Daadab inayowapa hifadhi maelfu ya wakimbizi kutoka nchini Somalia.

Matangazo ya kibiashara

Amnesty International inasema Kenya ina jukumu  kwa mujibu wa sheria za Kimataifa, kuwalinda wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi kutokana na sababu mbalimbali na hivyo uamuzi wa kufunga kambi hiyo sio sahihi kwa sasa.

Tume ya kitaifa ya kutetea haki za Binadamu nchini Kenya na wanaharakati wengine kama Kituo cha Sheria wanataka Mahakama kuamua kuwa uamuzi wa serikali ya Kenya ni kinyume cha katiba ya nchi hiyo, kwa sababu kufungwa kwa kambi hiyo itakuwa ni kinyume cha haki za binadamu.

Michelle Kagari Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Amnesty International Afrika Mashariki amesema uamuzi wa serikali ya Kenya utahatarisha usalama wa maelfu ya raia wa Somalia, ambao wanahofia kurudi nyumbani kutokana na tishio la kundi la kigaidi la Al Shabab lakini pia hawana pa kwenda.

Aidha, Amnesty International inaishtumu serikali ya Kenya kwa kuwalazimisha wakimbizi hao kurudi nyumbani kwa nguvu kinyume na sheria za Kimataifa, ambazo zinawataka wakimbizi kurejea makwao kwa hiari.

Serikali ya Kenya mwezi Mei mwaka huu ilitangaza kuwa kufikia mwisho wa mwezi Novemba mwaka huu, zaidi ya wakimbizi 260,000 wa Somalia wanaoishi katika kambi hiyo watarudishwa nyumbani kwa sababu za kiusalama.

Umoja wa Mataifa unaitaka pia Kenya kulegeza msimamo wake.