SUDAN KUSINI-UGANDA

Wakimbizi wa Sudan Kusini wanaoishi Kaskazini mwa Uganda wakosa maji

Wakimbi wa Sudan Kusini
Wakimbi wa Sudan Kusini Beatrice Mategwa/United Nations Mission in South Sudan (UNMISS)

Wakimbizi 190,000 raia wa Sudan Kusini wanaoishi katika kambi ya Bidibidi katika Wilaya ya Yumbe Kaskazini mwa nchi ya Uganda, wanakabiliwa na uhaba wa maji hali ambayo inaendelea kufanya maisha yao kuwa magumu.

Matangazo ya kibiashara

Wakimbizi hao wamekuwa wakiishi katika kambi hiyo baada ya kukimbia mapigano katika jimbo la Equatorial, hasa wale waliokuwa wanaishi katika miji ya Yei na Nimule.

Licha ya wakimbizi hao kupata msaada wa maji kutoka kwa Shirika la kimataifa la OXFAM, maji hayo hayawatoshi kutokana na idadi kubwa ya wakimbizi katika kambi hiyo.

Wakimbizi hao wanatumia muda wao mwingi kupanga foleni kujaribu kujipatia maji, huku wakimbizi hao sasa wakitaka wasaidiwe kwa kuchimbwa kwa mabwawa yatakayowasaidia kupata maji ya kutosha.

Mmoja wa wakimbizi hao Mary Akol amesema watoto wake hawawezi hata kuoga.

“Watoto wangu hawawezi kuoga kwa sababu maji kidogo tunayopata tunatumia kupikia chakula. Hali hii ni sawa na ile tuliyoshuhudia nyumbani,” aliongeza Mary.

Nasir Fernandes, afisa wa Shirika la kushughulikia wakimbizi UNHCR amesema wanachunguza suala hili kuwasaidia wakimbizi hao.