SUDAN KUSINI-KENYA

Raia wa Kenya waachiliwa huru na waasi nchini Sudan Kusini

Kiongozi wa waasi nchini Sudan Kusini Riek Machar
Kiongozi wa waasi nchini Sudan Kusini Riek Machar AFP Photo:UNMISS/Isaac Alebe Avoro

Waasi wa upinzani nchini Sudan Kusini (SPLM-IO) wanasema wapiganaji wake wamewaachilia huru raia wa Kenya waliokuwa wanafanya kazi ya kutoa misaada ya kibinadamu wakati walipokamatwa na kuzuiwa katika jimbo la Akobo.

Matangazo ya kibiashara

Wakenya hao 72 wamekuwa wakifanya kazi na mashirika mbalimbali ya Kimataifa yasiyokuwa ya kiserikali, kuwasaidia watu walioathirika na mapigano nchini humo.

Hatua hii imekuja baada ya msemaji wa kiongozi wa waasi Riek Machar, James Gatdet Dak kukamatwa na kusafirishwa kwa nguvu kutoka jijini Nairobi kwenda jijini Juba wiki iliyopita.

Goanar Gordon Yien, mmoja wa viongozi wa juu wa waasi hao hao ameliambia Gazeti la Sudan Tribune kuwa wakenya hao tayari wameshaachiliwa huru.

Yien amesema upande wa upinzani hauna uhakika ikiwa msemaji wa Machar yuko salama, na sasa unataka Umoja wa Mataifa na Muungano wa nchi za Afrika Mashariki IGAD kuhakikisha kuwa anakuwa salama na huru.

Upinzani unamshutumu Makamu wa kwanza wa rais Taban Deng, kutaka kurudishwa nyumbani kwa viongozi wengine wa upinzani 15 wanaoishi jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.