TANZANIA-HABARI

Tanzania: Rais Magufuli atia saini sheria ya huduma za habari

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, hatimaye ametia saini sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, sheria ambayo ilipitishwa wakati wa kikao cha bunge la 11 mjini Dodoma.

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, Dar es Salaam, Novemba 4, 2016.
Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, Dar es Salaam, Novemba 4, 2016. Screenshot/Azama TV
Matangazo ya kibiashara

Kutiwa saini kwa sheria hii, kunatamatisha safari ndefu ya mijadala na maoni kuhusu maboresho ya muswada huo, ambapo majuma kadhaa yaliyopita wakati akizungumza na wahariri kwenye ikulu ya Dar es Salaam, Rais Magufuli aliapa kutia saini sheria hiyo punde tu ikifika mezani kwake.

Punde baada ya kutia saini muswada huo wa huduma za habari kuwa sheria, rais Magufuli akawapongeza wadau wote walioshiriki kutoa maoni yao kuhusu kuboreshwa kwa muswada wenyewe ambapo wabunge waliupitisha kwa kauli moja mjini Dodoma.

Rais Magufuli amewapongeza wabunge kwa kuipitisha sheria hiyo ambapo amesema "Naamini kuwa Sheria hii itasaidia kuboresha sekta ya habari kwa manufaa ya wanataaluma wenyewe na Taifa". alimaliza Rais Magufuli.

Sheria hiyo hata hivyo inatiwa saini huku wadau wa habari wakiwa hawajaridhishwa na baadhi ya vipengele vilivyokuwemo, ambavyo wanasema vinaenda kuminya uhuru wa upashaji habari.

Baadhi ya wahariri waliozungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Radio France International, RFI, wamesema kuwa hawajafurahishwa na namna mchakato wenyewe ulivyokuwa na hata hatua ya rais kuamua kutia saini kuwa sheria rasmi.

Hata hivyo kwa upande mwingine wahariri hao wamepongeza baadhi ya vipengele vilivyokuwemo kwenye sheria hiyo, ambapo wanasema sasa taaluma ya uandishi wa habari itaheshimika kama zilivyo taaluma nyingine kuliko na ilivyokuwa awali.

Nao waandishi wa habari wa kawaida, mbali na kueleza kuguswa na kutiwa saini kwa sheria hiyo kabla ya kufanyika kwa marekebisho zaidi, wamepongeza pia baadhi ya vipengele vilivyomo ambavyo wanasema vitalinda maslahi yao, pamoja na kutoa nafasi kwa waandishi zaidi kwenda kusoma ili kuongeza ujuzi.

Kabla ya muswada wenywe kupelekwa bungeni, wadau walipata fursa ya kutoa maoni yao kwa kipindi maalumu, ingawa hawakuridhishwa na muwa waliopewa kutoa maoni licha ya muswada wenywe kufanyiwa marekebisho baada ya awali kuwa ulikataliwa bungeni.

Hii ina maanisha kuwa, waziri wa habari sasa atatoa tangazo kupitia gazeti la Serikali kuutarifu uma kuhusu kutiwa saini kwa sheria hiyo na kuanza kutumika rasmi.

Sheria hii bado imeendelea kukosolewa na wadau wa habari pamoja na mashirika ya kimataifa na yale ya ndani yanayotetea haki za binadamu, ambayo yanasema kuwa sheria hii licha ya mazuri yaliyomo, lakini mengi yanaenda kuminya uhuru wa kupata habari na kumpa mamlaka makubwa waziri, ambaye atakuwa na uwezo wa kukifungia kituo cha redio, gazeti au mtandao, ikiwa ataona habari waliyochapisha ina hatarisha usalama wa nchi au ni ya upotoshaji.