SUDAN KUSINI

Rais Kiir asema yuko tayari kumsamehe Machar ikiwa atatangaza kuacha vita

Rais Salva Kiir (Kushoto) akiwa na mpinzani wake na kiongozi wa waasi Riek Machar (Kulia)
Rais Salva Kiir (Kushoto) akiwa na mpinzani wake na kiongozi wa waasi Riek Machar (Kulia) REUTERS/Goran Tomasevic

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amesema mpinzani wake na kiongozi wa waasi Riek Machar hatapewa msamaha, ikiwa hataacha vita.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita, Kiir amemshtumu Machar kwa kutumia nguvu lakini pia kuwauawa wananchi wasiokuwa na hatia kutaka kuwa rais wa nchi hiyo.

“Nimemwambia ndugu yangu Machar kuwa njia pekee ya kuwa rais ni kusubiria uchaguzi, na si kutumia vita na kuwauwa wananchi wasiokuwa na hatua lakini hasikilizi,” alisema rais Kiir.

Aidha, amesema amepokea maombi ya watu wengi wanaomwomba amsamehe Machar wakati atakaporejea nchini.

“Watu wanakuja kwangu kuniomba nimsamehe Machar akirejea, mimi huwaambia sina shida naye, yeye ni raia wa nchi hii, anaweza kurejea wakati wowote lakini kikubwa atangaze kuwa anaacha vita,” aliongeza Kiir.

Tayari rais Kiir ametoa msamaha kwa wanajeshi 750 waliokuwa wanamuunga mkono Machar ambaye pia alikuwa Makamu wa kwanza wa rais.

Wapiganaji hao waliosamehewa ni wale waliotoroka na kiongozi wao Machar katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwezi Julai mwaka huu wakati mapigano mapya yalipozuka jijini Juba.

Riek Machar kwa sasa anaishi nchini Afrika Kusini.

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa huenda vita vipya vikazuka nchini Sudan Kusini na ikawa vigumu kwa vikosi vya Umoja huo kuvizuia.