BURUNDI-UN

Wananchi wa Burundi wapinga uchunguzi wa UN kuhusu ukiukaji haki

Maelfu ya raia wa Burundi jana Jumamosi wamepinga uchunguzi wa Umoja wa Mataifa katika madai ya ukiukwaji wa haki, hatua ambayo ni ya karibuni kuashiria hasira dhidi ya kile ambacho mamlaka zinaona ni kuingiliwa na nchi za kigeni katika taifa hilo. 

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza AFP PHOTO / STRINGER
Matangazo ya kibiashara

Ukosoaji wa kimataifa umeongezeka nchini Burundi kuhusu ukiukwaji wa haki tangu Rais Pierre Nkurunziza awanie muhula wa tatu mnamo Aprili 2015 na kushuhudia Burundi ikijiondoa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC.

Aidha Burundi imesitisha mahusiano na shirika kuu la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa baada ya kutoa ripoti ya ukiukaji mkubwa wa haki mnamo mwezi Septemba na kuonya kuhusu mauaji ya kimbari.

Ripoti hiyo ilisababisha baraza la usalama la umoja wa mataifa kutangaza mwaka mmoja wa uchunguzi kuhusu madai ya ukiukaji wa haki uliotekelezwa nchini Burundi tangu kuzuka kwa mgogoro wa kisiasa mwaka jana ambapo wajumbe wa tume ya uchunguzi kutoka Algeria, Benin na Uingereza waliteuliwa siku ya Jumanne kuongoza uchunguzi huo.

Meya wa jiji la Bujumbura Freddy Mbonimpa ametoa wito kwa umma kujitokeza kwa wingi kufanya maandamano makubwa kupinga uteuzi wa wataalamu watatu wa UN kwa ajili ya uchunguzi huo.