UGANDA

Mfalme wa Rwenzururu akamatwa, ahusishwa na mauaji ya watu 55

Mfalme wa eneo la Rwenzururu nchini Uganda mpakani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Charles Wesley Mumbere, anashikiliwa na maafisa wa usalama jijini Kampala.

Gari ya jeshi la Uganda ikiegeshwa kwenye mlima wa Rwenzori, karibu na kijiji cha Kichwamba (kusini magharibi mwa Uganda
Gari ya jeshi la Uganda ikiegeshwa kwenye mlima wa Rwenzori, karibu na kijiji cha Kichwamba (kusini magharibi mwa Uganda Gaël Grilhot/RFI
Matangazo ya kibiashara

Mfalme huyo anahojiwa ili kufahamu mengi kuhusu makabiliano ya mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya waasi kuvamia kituo cha Polisi mjini Kasese na baadaye kusababisha makabiliano makali ambayo yamesababisha vifo vya watu 55.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini humo Andrew Felix Kaweesi amethibitisha kushikiliwa kwa Mfalme huyo ambaye pia anatarajiwa kukutana na rais Yoweri Museveni.

Aidha, Polisi inasema ikiwa itabainika kuwa Mfalme huyo alihusika kwa kupanga au kuwahifadhi mavamizi hao, watafunguliwa mashtaka ya uhaini.

“Tunafanya uchunguzi, na ikiwa tutapata ushahidi dhidi ya Mfalme kuhusika kwa namna moja au nyingine, tutamfungulia mashtaka ya uhaini, ugaidi na mauaji,” amesema Kaweesi.

Polisi 14 waliuawa baada ya kukatwa kwa mapanga na kushambuliwa na silaha zingine kama vilipuzi kwa mujibu wa viongozi wa usalama nchini humo ambao wanasema baada ya uvamizi huo wa kituo cha Polisi, wavamizi hao walikwenda kujificha ndani ya Kasri la Mfalme huyo.

 

Mfalme wa Rwenzururu nchini Uganda,Charles Wesley Mumbere akiwa na Mkewe
Mfalme wa Rwenzururu nchini Uganda,Charles Wesley Mumbere akiwa na Mkewe www.redpepper.co.ug

Jeshi la UPDF lilishirikiana na Polisi kwa sasa linaendelea kupiga kambi katika maeneo ya Kasri hiyo huku zaidi ya walinzi wengine zaidi ya 40 wa Mfalme wakikamatwa.

Mfalme Mumbere, amekanusha kuhusika kwa namna yoyote ya machafuko hayo licha ya kuwepo kwa madai kuwa Ufalme wake kwa muda mrefu umekuwa ukitaka kujitawala na kujiondoa nchini Uganda.

Eneo la Kasese limekuwa likihusishwa kuwa chimbuko la waasi wa ADF NALU ambao kwa sasa wamekimbia nchini DRC, wanakoendelea kusababisha ukosefu wa usalama.

Katika hatua nyingine, Mwanahabari Joy Doreen Biira alikamatwa katika eneo hilo la makabiliano.

Polisi inasema raia huyo wa Uganda anayefanya kazi na kituo cha Televisheni nchini Kenya KTN, alikamatwa baada ya kwenda kinyume na maagizo ya maafisa wa usalama kutokaribia eneo la mapambano.

Inaelezwa kuwa anatarajiwa kuachiliwa huru baada ya kuhojiwa na polisi.