BURUNDI-RWANDA

Burundi yaishtumu Rwanda kwa kupanga kumuua msemaji wa rais Pierre Nkurunziza

Serikali ya Burundi, imeishtumu nchi jirani ya Rwanda kwa kupanga shambulizi dhidi ya msemaji wa rais Pierre Nkurunziza, Willy Nyamitwe.

Willy Nyamitwe, akihojiwa na mwanahari wa RFI Kifaransa  Sonia Rolley, hivi karibuni
Willy Nyamitwe, akihojiwa na mwanahari wa RFI Kifaransa Sonia Rolley, hivi karibuni Photo : RFI / Richard Riffonneau
Matangazo ya kibiashara

Mmoja wa mlinzi wake aliuawa na mwingine kujeruhiwa katika shambulizi hilo huku Nyamitwe akijeruhiwa mkononi na kwenda kupata matibabu.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Nyamitwe ameandika kuwa anaendelea vema lakini anaomboleza kifo cha mlinzi wake.

Msemaji wa Polisi nchini humo Pierre Nkurukiye, amesema watu waliokuwa wamejihami kwa silaha walipata maagizo kutoka Rwanda kumuua Nyamitwe.

Aidha, amesema baada ya shambulizi hilo wanajeshi wawili wa Burundi wamekamatwa kwa kuhusika katika shambulizi hilo lililotokea usiku wa kuamkia siku ya Jumanne.

Licha ya tuhma hizo, serikali ya Rwanda haijazungumzia tuhma hizo lakini imekuwa ikikanusha mara kwa mara kuhusika na machafuko nchini Burundi.

Uhusiano kati ya mataifa haya mawili umekuwa mbaya tangu jaribio la mapinduzi nchini Burundi mwaka 2015.

Burundi pia imekuwa ikiishtumu Rwanda kwa kuwapa mafunzo ya kijeshi wakimbizi wanaokimbilia katika nchi yake, ili kushambulia utawala wa rais Nkurunziza.