UGANDA-SIASA-USALAMA

Rais Museveni alimpigia simu Mfalme Mumbere bila mafanikio

Rais wa Uganda Yoweri Museveni alimpigia simu Mfalme wa Rwenzururu Charles Wesley Mumbere Jumapili iliyopita na kumtaka kuamuru walinzi wake kuweka silaha chini kabla ya kuzuka kwa makabiliano kati ya walinzi hao na maafisa wa usalama.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri Museveni ©Gaël Grilhot/RFI
Matangazo ya kibiashara

Baada ya mazungumzo hayo kutozaa matunda, jeshi la UPDF likishirikiana na polisi lilivamia Kasri ya Mfalme huyo na kuanza makabiliano makali ambayo yamesababisha vifo vya watu 62 wakiwemo maafisa wa polisi.

Brigedia Peter Elweluthe amesema, Mfalme huyo alipewa muda wa saa moja kuzungumza na walinzi wake na kuwataka kuweka silaha chini lakini agizo la rais Museveni halikuheshimiwa.

“Tulimpa muda wa saa moja lakini hakufanya lolote. Rais akampigia tena na kumpa muda mwingine wa saa mbili na kumwomba kushughulikia suala hili,” aliongeza Elweluthe.

“Hatukuwa na lingine bali kuvamia Kasri yake ili kuwaondoa hawa magaidi.”

Waziri wa Mambo ya ndani Jeje Odongo amemshtumu Mfalme Mumbere kwa kutaka kuanzisha vita, madai ambayo ameyakanusha.

Mfalme Mumbere anaendelea kuzuiliwa na polisi mjini Jinja wakati huu usalama ukiendelea kuimarishwa mjini Kasese.

Mashirika ya kutetea haki za Binadamu Human Rights Watch na Amnesty International, yameshtumu mauaji yaliyotokea na kutaka uchunguzi wa kina kufanyika kubaini kilichotokea.

Katika hatua nyingine, Mwanahabari wa Televisheni ya KTN nchini Kenya ambaye ni raia wa Uganda Joy Doreen Biira, aliyeachiliwa huru baada ya kukamatwa katika eneo la mapigano, amefunguliwa mashtaka ya kushirikiana na ugaidi.