SUDAN KUSINI

UN yaonya kuhusu kutokea kwa mapigano ya kikabila nchini Sudan Kusini

Wakaazi wa Malakal waliokimbia makwao katika siku zilizopita
Wakaazi wa Malakal waliokimbia makwao katika siku zilizopita Justin LYNCH / AFP

Watalaam wa maswala ya Haki za Binadamu kutoka Umoja wa Mataifa, wanaonya kuwa mapigano ya kikabila huenda yakashuhudiwa nchini Sudan Kusini.

Matangazo ya kibiashara

Mmoja wa watalaam hao Yasmin Sooka amesema mapigano haya yataanza kushuhudiwa kipindi cha ukame kinapoanza kushuhudiwa.

Matamshi haya yamekuja baada ya ziara ya siku 10 ya watalaam hao katika majimbo ya Bentiu, Malakal na Wau kuthathmini hali ya kiusalama.

“Nimesikia watu kutoka makabila mbalimbali wakisema kuwa wanapanga kulipiza kisasi kutoka na mzozo wa hivi karibuni,” alisema Sooka.

Mzozo wa Sudan Kusini ulianza miaka mitatu iliyopita baada ya rais Salva Kiir kumtuhumu aliyekuwa Makamu wake Riek Machar kwa kujaribu kumpindua kijeshi.

Licha ya mzozo huo kujaribu kutatuliwa na mkataba wa amani kufikiwa, mapigano mapya yalizuka mwezi Juni mwaka huu jijini Juba na kusababisha Machar kuikimbilia Afrika Kusini.

Watalaam hao wameitaka Jumuiya ya Kimataifa kuiwekea vikwazo serikali ya Juba kununua na kuingiza silaha nchini humo lakini pia kutuma haraka iwezekanavyo kikosi cha wanajeshi wa ukanda wapatao 4,000 kulinda amani nchini humo hasa jijini Juba.