KENYA

Madaktari wagoma nchini Kenya wataka nyongeza ya mshahara

Madaktari na wahudumu wengine wa afya katika Hospitali za Umma nchini Kenya, wanagoma kuishinikiza serikali kutekeleza makubaliano ya nyongeza ya mshahara kama walivyokubaliana mwaka 2013.

Mmoja wa Madtari wakati wa maandamano Desemba 5 2016 jijini Nairobi
Mmoja wa Madtari wakati wa maandamano Desemba 5 2016 jijini Nairobi Reuters
Matangazo ya kibiashara

Mgomo huu umetatiza huduma za afya katika hospitali za serikali huku wagonjwa wakikosa huduma na wasio na uwezo kulazimika kurudi nyumbani.

Chama cha Madaktari nchini humo KMPDU kinasema, hakuna Daktari atakayerudi kazini hadi pale serikali itakapotekeleza makubaliano hayo kikamilifu.

Katibu Mkuu wa chama hicho Fredrick Oluga amesema mgomo huo umekuja baada ya Madaktari na wahudumu wengine wa afya kuona kuwa serikali haishughulikii madai yao hata baada ya kutoa makataa ya siku 21.

Madaktari wanaitaka serikali kutekeleza makubaliano hayo ya kuwaongezea mshahara kwa asilimia 300 kwa mujibu wa mkataba uliotiwa saini mwaka 2013.

Suala lingine ambalo Madaktari hao wanadai ni pamoja na kupewa mafunzo zaidi na kuwaajiri wahuduma zaidi wa afya katika Hospitali za umma.

Juhudi za serikali kupitia Wizara ya afya kuzugumza na chama cha Madaktari na wahudumu wengine wa afya hazikufua dafu baada ya kutofika katika mkutano wa pamoja siku ya Jumapili usiku.

Magavana wa majimbo 47 licha ya kwenda Mahakamani, kutaka mgomo huo kusitishwa, hatua hiyo pia haikufua dafu na sasa haifahamiki mgomo huo utaisha lini.

Serikali inasema iko tayari kutekeleza mkataba huo kwa awamu, huku Magavana wa majimbo wakisema watawaajiri Madaktari wegine kufanya kazi kwa muda ambao mgomo huu utaendelea.

Wakati mgomo huo ukiendelea, baadhi ya wagonjwa katika Hospitali ya watu wanaosumbuliwa na magonjwa ya akili walifanikiwa kutoroka baada ya kukosa madakatri na wahudumu wengine wa afya kuwapa huduma.