ICC-LRA-UGANDA

Kesi ya Kamanda wa LRA Dominic Ongwen yaanza ICC

Kesi dhidi ya Kamanda wa zamani wa kundi la Lord Resistance Army nchini Uganda ,Dominic Ongwen inaanza leo katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC mjini Hague nchini Uholanzi.

Dominic Ongwen Kamanda wa kundi la LRA akiwa katika Mahakama ya ICC mjini Hague nchini Uholanzi
Dominic Ongwen Kamanda wa kundi la LRA akiwa katika Mahakama ya ICC mjini Hague nchini Uholanzi PETER DEJONG / POOL / AFP
Matangazo ya kibiashara

Ongwen ameshtakiwa kwa makosa 70 ya uhalifu wa kivita dhidi ya Binadamu, ikiwa ni pamoja na  mauaji, ubakaji na utekwaji wa watoto wakati akishirikiana na kiongozi wake Joseph Kony ambaye bado anatafutwa.

Mshukiwa huyu mwenye umri wa miaka 40, alijiunga na LRA akiwa mtoto mwenye umri wa miaka 14 Kaskazini mwa Uganda.

Anakuwa mmoja wa viongozi wakuu wa LRA kushtakiwa katika Mahakama hiyo ya Kimataifa, huku makamanda wengine wakiongozwa na Joseph Kony na  Vincent Otti  wakiendelea kutafutwa.

Mashahidi zaidi ya 4,000 wengi wao wakiwa ni watu walioteswa na kutekwa na kundi hilo la LRA, wantarajiwa kutoa ushahidi wao dhidi ya Ongwen, katika kesi hii muhimu ambayo inafuatiliwa kwa karibu hasa Kaskazini mwa Uganda.

Ogwen alikamatwa mwezi Januari mwaka 2015 na waasi wa Seleka katika misitu ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, kabla ya kukabidhiwa kwa jeshi la Marekani, lililomsafirisha nchini Uganda na baadaye akafikishwa ICC.

Tangu kuanzishwa kwa kundi la LRA mwaka 1987, Umoja wa Mataifa unasema, kundi hilo limewauawa zaidi ya watu 100,000 na kuwateka zaidi ya watoto 60,000 Kaskazini mwa Uganda na mataifa mengine jirani kama Sudan, DRC na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Kundi hili liliundwa ili kupindua uongozi wa rais Yoweri Museveni miaka 30 iliyopita.