KENYA

Serikali na Madaktari nchini Kenya wakutana kujaribu kumaliza mgomo unaoendelea

Madaktari nchini Kenya wakiandama jijini Nairobi Desemba 5 2016
Madaktari nchini Kenya wakiandama jijini Nairobi Desemba 5 2016 Reuters

Mgomo wa Madaktari na wahudumu wengine wa afya nchini Kenya unaendelea kwa siku ya pili.

Matangazo ya kibiashara

Gazeti la kila siku nchini humo Daily Nation limeripoti kuwa wagonjwa saba wamepoteza maisha baada ya kukosa matibabu katika hospitali mbalimbali za umma .

Maafisa wa serikali pamoja na wawakilishi wa Madaktari wanakutana kwa dharura kujaribu kupata mwafaka kuhusu madai ya Madaktari hao.

Madakatari na wahudumu wengine wa afya wanagoma kushinikiza serikali kutekeleza makubaliano ya nyongeza ya mshahara kwa asilimia 300 kama ilivyokubaliwa mwaka 2013 na wanataka matakwa yao kushughulikiwa kabla ya kurejea kazini.

Aidha, wanataka uboreshaji wa mazingira ya kufanya kazi na wahudumu wa afya kupewa mafunzo zaidi.

Nao Madkatari wengine wenye vyeti vya Diploma na wasiofanya upasuaji, wanatarajiwa kuanza kugoma siku ya Jumatano.

Naibu Katibu Mkuu wa Madaktari hao Austine Oduor ameiambia RFI Kiswahili kuwa, wanataka serikali kutambua muungano wao, kuwalipa wanafunzi wanaojifunza kazi lakini pia kuongezewa mshahara.

"Tupo zaidi ya 20,000 hapa nchini Kenya tunashangaa ni kwanini serikali haitaki kututambua kama ilivyo kwa Manesi na wahudumu wengine wa afya," alisema Oduor.

"Tutakutana jijini Nairobi siku ya Alhamisi kujadili maswala yetu," aliongeza.

Serikali ya Kenya inasema kutokana na changamoto za kifedha itaweza tu kutekeleza makubalino hayo kwa hatua.

Katika hatua nyingine, Polisi wameanza msako wa kuwatafuta wagonjwa wenye akili waliotoroka katika Hospitali ya Mathare jijini Nairobi siku ya Jumatatu baada ya kuanza kwa mgomo huo.