KENYA

Rais Kenyatta asema Mataifa ya nje yanaingilia siasa za Kenya

Rais Uhuru Kenyatta wakati wa wimbo wa taifa wakati wa maadhimisho ya miaka 53 ya Jamhuri Day jijini Nairobi Desemba 12 2016
Rais Uhuru Kenyatta wakati wa wimbo wa taifa wakati wa maadhimisho ya miaka 53 ya Jamhuri Day jijini Nairobi Desemba 12 2016 myuhurukenyatta/photos

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, ameyaonya mataifa ya kigeni kuacha kuingilia na kushawishi siasa za nchi hiyo  kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka ujao.

Matangazo ya kibiashara

Akilihotubia taifa katika maadhimisho ya miaka 53 ya Jamhuri, siku ambayo taifa hilo lilipoanza kijitawala katika sherehe zilizofanyika jijini Nairobi na kuhudhuriwa pia na rais wa Togo Faure Gnassingbé,  rais Kenyatta amesema ikiwa mataifa hayo ya kigeni ambayo hakuyataja yanataka kuisaidia Kenya, yaitumie Tume ya Uchaguzi.

“Wakenya wanafahamu namna ya kupiga kura na ndio watakaoamua wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka ujao, “ alisema Kenyatta.

“Kama wanataka kutusaidia, watumie Tume ya Uchaguzi sio kuzunguka kila mahali nchini,” aliongeza.

VICTOR ABUSO RIPOTI KUHUSU SHEREHE ZA JAMHURI MIAKA 53

Pamoja na hilo, amewataka wanasiasa kufanya kampeni kwa utulivu na kuepuka matamshi yanayoweza kuligawa taifa hilo ili kusababisha machafuko yaliyotokea baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007.

“Nawaomba wanasiasa, waombe kura kwa amani na kuwaeleza wananchi sera zao ili wafanye maamuzi “.

Kuhusu Mahakama ya Kimataifa ya ICC, rais Kenyatta amesema huu ndio wakati wa nchi yake kuanza kufikiria ikiwa itaendelea kuwa mwanachama wa Mahakama hiyo au la.

“Tulichopitia katika Mahakama ya ICC, kilituonesha wazi kuwa Mahakama hiyo sio huru. Tumeanza kuyaona mataifa mengi yakionesha nia ya kujiondoa na mengine yakijiondoa,".

"Mapendekezo ya kuiboresha Mahakama hii hayajafanyiwa kazi, kwa hivyo, itabidi tufikirie sana kuhusu uanachama wetu katika Mahakama hii,”.

Kenyatta alifikishwa katika Mahakama hiyo kwa madai ya kuhusika na machafuko ya baada ya Uchaguzi wa mwaka 2007, lakini kesi yake ikafutwa baada ya kukosekana kwa ushahidi.

Mataifa mengi ya Afrika yamesema yanataka kujiondoa katika Mahakama hiyo kwa madai kuwa yanawaonea viongozi wa Afrika.