TANZANIA

Mwanzilishi wa mtandao wa Jamii Forums nchini Tanzania akamatwa

Mkurugenzi na mwanzilishi wa mtandao wa kijamii wa Jamii Forums Maxence Melo.
Mkurugenzi na mwanzilishi wa mtandao wa kijamii wa Jamii Forums Maxence Melo. www.jamiiforums.com

Mkurugenzi na mwanzilishi wa mtandao wa kijamii wa Jamii Forums Maxence Melo, anashikiliwa na polisi kwa tuhma za kukwamisha upelelezi wa makosa ya mtandao.

Matangazo ya kibiashara

Polisi wanasema Melo baada ya kuhojiwa amekataa kutoa ushirikiano kuhusu wachangiaji wa mtandao huo.

Wakili wake Benedict Ishabakaki amethibitisha kukamatwa kwa mteja wake ambaye hakufikishwa Mahakamani jijini Dar es salaam kama ilivyotarajiwa siku ya Jumatano.

Tangu kuanzishwa kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 nchini humo, Jeshi la Polisi limekuwa likiushinikiza mtandao huo kutoa taarifa za baadhi ya wateja wake.

Hata hivyo, JamiiForums imekuwa ikihoji shinikizo kutoka Polisi na kutaka kujua sheria wanayotumia kutaka kuwekwa wazi kwa wachangiaji wa mtandao huo.

Mtandao wa JamiiForums tayari umekwenda Mahakamani kutaka vifungu vya sheria hiyo kutaka vibadilishwe kwa madai kuwa vinakeuka haki ya Watanzania ya kujieleza kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo.