SUDAN KUSINI

UNSC yaongeza mwaka mmoja kwa kikosi cha UNIMISS Sudan Kusini

Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa
Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa UN Photo/Loey Felipe

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana Ijumaa limeongeza muda wa ujumbe wake wa kulinda amani nchini Sudan Kusini kwa mwaka mmoja, ukitaka kumaliza mapigano nchini humo wakati vita hiyo ikiingia mwaka wake wa nne. 

Matangazo ya kibiashara

Baada ya siku moja ya mazungumzo magumu, baraza kwa kauli moja lilipitisha azimio lililoandaliwa na Marekani kwamba kikosi cha UNIMISS chenye askari elfu 14, kiongezewe muda hadi Desemba 2017.

Kwa mujibu wa hatua hiyo, ujumbe huo utajumuisha kikosi kipya cha kikanda chenye askari 4,000, ambao baraza liliamua wapelekwe nchini humo mwezi Agosti lakini hadi sasa bado hawajakanyaga ardhi ya Sudan Kusini.

Azimio hilo linatishia vikwazo dhidi ya wale ambao wanadhoofisha utulivu wa Sudan Kusini na kuonya kuwa baraza litazingatia "hatua mwafaka" ikiwa ni pamoja na vikwazo vya silaha kushughulikia hali inayojiri.

Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Samantha Power ameelezea hatua hiyo kama namna ya kuboresha kikosi cha UNMISS, ambacho kimekuwa kinakosolewa kwa kushindwa kulinda raia wakati wa miaka mitatu ya vita.

Urusi, China, Venezuela na nchi tatu za Afrka katika baraza la Usalama zilipinga mwenendo wa Marekani katika kushughulikia mzozo wa Sudan Kusini , na kupinga vikwazo vya silaha.

Kwa upande wake katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amewakosoa viongozi wa Sudan Kusini na kusema wamesaliti imani ya watu wao na kuvunja makubaliano ya amani.