KENYA

Wanasiasa nchini Kenya wazozana kuhusu mabadiliko ya sheria ya Uchaguzi

Mzozo wa kisiasa unashuhudiwa nchini Kenya kati ya wabunge wa serikali na wale wa upinzani kuhusu mabadiliko ya sheria za Uchaguzi.

Bunge la Kenya
Bunge la Kenya kenyan-parliament
Matangazo ya kibiashara

Kenya inatarajiwa kuwa na Uchaguzi Mkuu mwezi Agosti mwaka 2017, uchaguzi ambao rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuwania tena kwa muhula wa pili dhidi ya mgombea wa muungano wa upinzani ambaye bado hajafahamika.

Wabunge wa serikali wanataka sheria ya uchaguzi inayotaka matokeo ya urais kujumuishwa kwa mfumo wa kieletroniki kubadilishwa kwa hofu kuwa huenda siku ya kupiga kura mtandao ukasumbua.

Aidha, wanataka mfumo wa kuwatambua wapiga kura kwa mfumo huo pia usitegemewe na badala yake mfumo wa kawaida pia uruhusiwe kwa tahadhari mabadiliko ambayo wanasiasa wa upinzani wanapinga.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amewaambia wabunge wake kutounga mkono mabadiliko hayo kwa madai kuwa, serikali inataka kutumia mabadiliko hayo kuiba kura.

Upande wa serikali nao unadai kuwa upinzani nao unataka kutumia mfumo huo wa teknolojia kwa usaidizi wa mataifa ya nje ili kuiba kura.

Wabunge wa upinzani walifika bungeni mapema siku ya Jumanne jijini Nairobi na kuzuia lango kuu la kuingia bungeni na kufanikiwa kumzuia Spika Justin Muturi kufika katika majengo ya bunge.