KENYA

Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Kenya wamtaka rais Kenyatta kuyakataa mabadiliko ya sheria ya Uchaguzi

Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Kenya
Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Kenya www.kccb.or.ke

Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Kenya, wanamtaka rais Uhuru Kenyatta kutotia saini mabadiliko ya sheria ya Uchaguzi, yaliyopitishwa na wabunge wa serikali siku ya Alhamisi.

Matangazo ya kibiashara

Aidha, wamesema, hatua hii itatoa nafasi ya mazungumzo kati ya serikali na upinzani ili kupata mwafaka wa pamoja kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2017.

Aidha, Kanisa Katoliki limetoa wito kwa muungano wa vyama vya upinzani nchini humo CORD kutoa nafasi ya mazungumzo ili kujaribu kutatua mzozo huu.

Hatua hii imekuja baada ya kinara wa upinzani Raila Odinga ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani, kutangaza kuwa muungano wa upinzani utakuwa na maandamano tarehe 4 mwezi Januari mwaka 2017, kupinga mabadiliko hayo.

Mabadiliko hayo yanatoa fursa kwa Tume ya Uchaguzi kutumia mbinu mbadala ya kujumuisha matokeo na kuwatambua wapiga kura ikiwa mfumo wa Eletroniki, utakumbwa na hitilafu.

Upinzani unasema mabadiliko hayo yanayoungwa mkono na serikali yanalenga kumsaidia rais Kenyatta kushinda Uchaguzi mwaka ujao.

Tume ya Uchaguzi inasema imesikitishwa kuwa wanasiasa wa serikali na upinzani hawajakubaliana na kuhusu mabadiliko haya.