Jela kuu la Kigali lawaka moto
Imechapishwa:
Jela kuu la Kigali lililojengwa mwaka 1930 na kupewa jina la 1930 limewaka moto na hadi Jumapili hii jioni moto umekua ukiendelea kusambaa katika majengo mbalimbali ya gerea hilo. Mpaka sasa hijajulikana sababu ya tukio hilo.
1930 ni jela wanakozuiliwa wafungwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na wafungwa wa kisiasa na wale wanaoshtumiwa kuhusika katika mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini humo mwaka 1994. Victoire Ingabire, mpinzani wa kisiasa wa Paul Kagame ni miongoni mwa wanasiasa wanaozuiliwa katika jela hilo. Bi Ingabire alihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela miaka 4 iliyopita kwa tuhuma za kuchochea utengano wa kikabila na kuhatarisha usalama wa raia.
Viongozi mbalimbali serikalini wamewasili kwenye eneo la tukio ikiwa ni pamoja na mawaziri pamoja na wakuu wa jeshi na polisi.
Shughuli za kuzima moto bado zinaendelea huku vikosi vya jeshi na polisi vikionekana pembezoni mwa jengo la gereza hilo.
Waandishi wa habari bado wamezuiliwa kukaribia katika eneo la tukio, na ni vigumu kujua kinachoendelea katika eneo hilo.
Maafisa wa zima moto bado wanaendelea kusafirisha majeruhi huku jeshi na polisi vikionekana vimezingira wafungwa ambao kwa sasa wamewekwa nje ya gereza na ulinzi ukiwa umeimarishwa.